

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Patrick Kenan Sawalla, tarehe 6 Agosti 2025, ametembelea banda la Bandari ya Mtwara katika maonesho ya 12 ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Ngongo vilivyopo Mkoani Lindi.
Mhe. Sawalla amevutiwa na utaratibu unaotumika kutoa elimu ya masuala ya Bandari kwa wadau mbalimbali wanaotembelea banda hilo. Vilevile, amesisitiza kuendelea kujiweka tayari katika kuhudumia shehena ya korosho katika msimu wa mwaka 2025/26.

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Namibia (NAMPORT) ambao upo Nchini kwa ziara ya mafunzo ya siku mbili, ukiwa na lengo la kujifunza kuhusu Shughuli za utekelezaji Bandarini na utendaji wa kimajukumu wa TPA.
Ujumbe huo wa Maafisa 13 kutoka NAMPORT, umeongozwa na Afisa Rasilimali Watu Mkuu Bi. Johana Hatutale na umepokelewa na Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa TPA Dkt. George Fasha kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Bw. Plasduce Mbossa.
Maafisa hao pia wamepata fursa ya kujifunza kuhusu usimamizi wa rasilimali watu, uboreshaji wa miundombinu ya Bandari na mbinu bora za utoaji huduma kwa wateja na pia utatembelea Chuo cha Bandari (Bandari College) kwa ajili ya kuona namna Tanzania inavyowekeza katika maendeleo ya rasilimali watu kwa ajili ya sekta ya bandari.
Ziara hii ni sehemu ya ushirikiano wa kimataifa wa TPA katika kubadilishana uzoefu, kukuza ufanisi na kuendeleza diplomasia ya bandari Barani Afrika.

Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Kayanza Pinda amewaasa wafanyabiashara wa mazao ya kilimo nchini kutumia Bandari ya Tanga kusafirsha mazao yao kwenda kwenye Soko la Kimataifa.
Mhe. Pinda aliyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki 2025, yanayojumuisha Mikoa minne ya Tanga, Dar es Salama, Pwani na Morogoro yanayofanyika katika Uwanja wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere maarufu kama “Viwanja vya NaneNane”.
“Bandari ya Tanga inatupa heshima sana katika nchi yetu hivyo natoa rai kwa wafanyabiashara wa mazao ya kilimo nchini kutumia Bandari hiyo ambayo imeboresha huduma zake” aliongeza Mhe Pinda.
Aidha Mhe. Pinda alitoa wito kwa Shirika la Reli la Tanzania (TRC ) na Bandari ya Tanga kuendelea kushirikiana ili kupanua wigo katika utoaji wa huduma katika sekta ya usafirishaji kanda ya mashariki.
Maonesho ya NaneNane Kanda ya Mashariki, kwa mwaka 2025 yanashirikisha Taasisi za umma na binafsi na Bandari ya Tanga ni mshiriki wa maonesho hayo ambayo yenye kauli mbiu ya “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025”.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) Dkt.Ladislaus Chang’a ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa ufanisi na uweledi katika kuhudumia Shehena.
Dkt.Chang’a ametoa kauli hiyo Agosti 04,2025 alipotembelea banda la TPA lililopo katika Viwanja vya Nzuguni Dodoma yanakofanyika Maonesho ya Wakulima (Nanenane)
Banda la TPA limekuwa kivutio katika Maonesho hayo yanayotarajiwa kufikia kilele Agosti 08, 2025 kwa watu wa rika tofauti kutembelea kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yahusuyo sekta ya Uchukuzi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Julai 31,2025, ameweka jiwe la msingi la uzinduzi wa Bandari Kavu ya Kwala iliyopo Vigwaza, Kibaha Mkoa wa Pwani.
Bandari hiyo ya kitaifa na kikanda imejengwa katika eneo lenye ukubwa wa hekta 502 ambapo kati ya hizo hekta 120 zimesafishwa na hekta tano zimejengwa kwa kiwango cha zege zikiwa ndani ya eneo la hekta 60 zilizozungushiwa uzio wenye urefu wa kilometa 2.96.
Bandari kavu ya Kwala inatarajiwa kuhudumia na kuhifadhi shehena ya makasha 3500 kwa siku na idadi ya makasha zaidi ya 300,000 kwa mwaka ikiwa ni takribani Asilimia 30 ya Makasha yote yanayopita katika Bandari ya Dar es Salaam.
Bandari hiyo itahudumia pia nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( DRC), Zambia, Malawi, Burundi, Rwanda na Uganda, ambapo nchi zote hizo zimepatiwa maeneo ndani ya Bandari Kavu hiyo ya Kwala.
- TPA YA SAINI MAKUBALIANO YA TARATIBU ZA UENDESHAJI WA KAWAIDA (SOP's) KWA AJILI YA UHAMISHAJI WA SHEHENA HADI KWALA
- TIMU ZA MPIRA WA WAVU YA TPA ZIMESHIRIKI UFUNGUZI WA LIGI YA MPIRA WA WAVU TAIFA (TVNL)
- WAZIRI WA UCHUKUZI AZUMGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI MAKAO MAKUU YA TPA KUHUSU UZINDUZI WA BANDARI KAVU YA KWALA
- MENJIMENTI YA TPA NA TRC YATEMBELEA BANDARI KAVU YA KWALA IKIWA NI UKAGUZI WAMAADALIZI YA UZINDUZI NA MHE. RAIS DKT SAMIA SULUHU HASSAN