

Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abed G. Abed ameongoza kikao cha siku moja kilichokutanisha maofisa wa DP Word na Chama cha Mawakala wa Meli kujadili changamoto mbalimbali katika shughuli za Kibandari za kila siku kwa lengo la kuongeza ufanisi katika kuhudumia meli katika Bandari ya Dar es Salaam

Bandari ya Mtwara imeendelea kupata pongezi kutoka kwa Wadau mbalimbali waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa Sekta ya Madini, kufuatia maboresho mbalimbali yaliyofanyika katika miundombinu, mifumo na vitendea kazi ili kuongeza ufanisi na utendaji kazi wa Bandari.
Pongezi hizo zimetolewa katika maonesho ya Madini na Fursa za Uwekezaji Mkoa wa Lindi yaliyofunguliwa rasmi tarehe 11 Juni 2025 na Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Shaib Hassan Kaduara.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw. Plasduce Mkeli Mbossa, amesema Bandari za Tanzania zina nafasi kubwa ya kuchangia katika mapato ya nchi na kukuza uchumi kutokana na maboresho makubwa ya miundombinu na uendeshaji yanayoendelea kufanyika.
Bw. Mbossa amebainisha hayo katika kipindi cha TUNATEKELEZA cha TBC1, akitilia mkazo kwamba, sekta binafsi kama DP World na Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited (TEAGTL) wameleta mageuzi makubwa ya utendaji na ufanisi katika Bandari ya Dar Es Salaam kinyume na hofu iliyokuwepo awali.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw. Plasduce Mkeli Mbossa, akiwa Katika kipindi cha TUNATEKELEZA kupitia TBC 1, akitolea ufafanuzi wa masuala kadhaa kuhusu mageuzi makubwa yanayofanyika katika uendeshaji wa Bandari nchini, tarehe 11 Juni,2025

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezipongeza Taasisi, Mashirika ya Umma ikiwemo Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Kampuni ambazo Serikali inamiliki hisa, kwa utendaji makini na kuonyesha kuridhishwa kwake na mwenendo ambao ni matokeo ya utekelezaji wa maelekezo yake kwa Taasisi na Mashirika ya Umma kuongeza tija na ufanisi katika utendaji.
Mhe. Rais ametoa pongezi hizo tarehe 10 Juni, 2025, Ikulu Jijini Dar es Salaam, katika hafla ya kupokea Gawio la Asilimia 15 ya Mapato ghafi ya Taasisi na Mashirika ya Umma kwa mwaka 2025 ambapo TPA imeibuka kinara katika Taasisi zinazotoa gawio la Asilimia 15 ya mapato ghafi kwa kutoa gawio la Shilingi bilioni 181.5 kutoka Shilingi bilioni 153.917 mwaka 2024.
Huu ni mwaka wa tatu mfululizo kwa TPA kuibuka kinara kwa kutoa gawio kwa Serikali, jambo linalotajwa kuchangiwa na ushirikishwaji wa sekta binafsi ikiwemo DP World na Tanzania East Africa Gateway Terminal katika uendeshaji wa shughuli za Bandari.