

Umoja wa Wanawake Wanaofanya kazi Sekta ya Bahari Mashariki na Kusini mwa Afrika (WOMESA) wametembelea Bandari ya Tanga na kuridhishwa na utendaji kazi katika bandari hiyo baada ya kukamilika kwa mradi wa maboresho ya bandari.
Akiongea wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Umoja huo Mhandisi Fortunata Makoye Kakwaya amesema kuwa, maboresho hayo yameleta mapinduzi makubwa katika bandari hiyo ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo meli kubwa zilikuwa haziwezi kufunga gatini kutokana na changamoto ya kina cha maji kuwa kifupi.
“Sisi Kama wadau katika sekta ya bahari maboresho haya yameleta mapinduzi makubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na kuifanya bandari hii ikidhi viwango vya Kimataifa katika uhudumiaji wa Meli na mizigo.
Aidha Bw. Gwakisa Mwaibuji, Afisa Mkuu Utekelezaji akiongea kwa niaba ya Meneja wa Bandari, Bw. Masoud Mrisha aliwaomba wadau hao kuwa mabalozi wazuri wa Bandari ya Tanga ili bandari hiyo iendelee kupokea shehena kubwa zaidi na mapato makubwa.

PUMZIKA KWA AMANI
Mhe. Cleopa David Msuya
Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu.
1931-2025

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imepokea tuzo maalum ya pongezi kwa mchango wake mkubwa katika kuzifanya Bandari za Tanzania kuwa miongoni mwa bandari shindani zaidi katika Ukanda wa mashariki na kusini mwa Bara la Afrika.
Tuzo hiyo imetolewa tarehe 9 Aprili,2025 jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa Chama cha Wataalam wa Lojistiki na Usafirishaji Tanzania (TALTA), hafla iliyohudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya uchukuzi kutoka ndani na nje ya nchi.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, amesema uzinduzi wa TALTA ni hatua muhimu katika kuimarisha weledi, uwajibikaji na utoaji wa huduma bora katika sekta ya uchukuzi nchini.
Ameeleza kuwa serikali inaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa kwenye miundombinu ya uchukuzi ikiwemo reli, barabara, bandari, viwanja vya ndege na vyuo vya mafunzo, hivyo kunahitajika wataalamu waliobobea kushirikiana na serikali katika maendeleo hayo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Usafiri kutoka Wizara ya Uchukuzi, Bw. Andrew Magombana, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, ameahidi ushirikiano wa karibu kati ya wizara na TALTA katika kutekeleza sera, mikakati na maboresho ya sekta hiyo muhimu.
Rais wa TALTA, Bw. Alphonce Mwingira, amesema dhamira ya chama ni kuwaunganisha wataalam wa fani ya lojistiki na usafirishaji kutoka ngazi zote za elimu na kushirikiana kwa karibu na Serikali pamoja na sekta binafsi katika kukuza taaluma hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TALTA, Dkt. Bartholomeo Lufunji, amesisitiza kuwa chama kitaendeshwa kwa kuzingatia maadili, sheria na kufanya tafiti kama nguzo kuu ya ufanisi wa sekta ya uchukuzi.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na wawakilishi kutoka Taasisi za Serikali, sekta binafsi, vyama vya usafirishaji, madereva, wamiliki wa magari ya abiria, na wanafunzi wa vyuo mbalimbali, tuzo mbalimbali zimetolewa kwa Viongozi wakuu wa kitaifa, Wizara, Taasisi za Umma na binafsi kwa kutambua mchango wao katika maendeleo ya sekta ya lojistiki na usafirishaji nchini.

Serikali ya Jamhuri ya Msumbiji imeeleza nia yake ya kuendeleza na kukuza ushirikiano uliopo baina yake na Tanzania haswa katika sekta ya Uchukuzi kupitia Ushoroba wa Kusini.
Hayo yamejiri katika Mkutano baina ya Waziri wa Uchumi na Uchukuzi wa Msumbiji Mhe. Basilio Muhate na Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) uliofanyika Mei 06,2025 Makao Makuu ya TPA jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika Mkutano huo Mhe.Muhate amesema ushirikiano katika sekta ya Uchukuzi baina ya nchi hizi utaunganisha Bandari za Mtwara na Nacala hali itakayosaidia ukuaji wa Uchumi wa nchi zote mbili.
Waziri huyo amesema nchi yake ina miundombinu ya kutosha inayoweza kutumika ipasavyo katika shughuli za Uchukuzi wa shehena kupitia Ushoroba wa Kusini.
Awali wakati akitoa salamu za ukaribisho kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Naibu Mkurugenzi Mkuu Dkt.Baraka Mdima, amesema shehena katika Bandari za Tanzania zinasafirishwa kwa njia ya Barabara na reli za TAZARA na Shirika la Reli la Tanzania (TRC) na mchakato wa ujenzi wa gati la kuhudumia meli za kitalii katika Bandari ya Dar es Salaam, upo katika hatua za mwisho.