

Wakuu wa Taasisi mbalimbali za Umma kwa nyakati tofauti wametembelea Banda la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA) katika Maonesho ya 32 ya Wakulima (Nanenane) yanayofikia tamati leo katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma na kuipongeza Mamlaka kwa ufanisi na mchango wake kwa Taifa kiuchumi.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) CPA Habibu J. Suluo ametoa pongezi zake kwa kusema wanatambua na kuthamini mchango wa TPA katika uchumi na kijamii.
Naye Kamishna wa Bima kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Dkt. Baghayo Saqware,amesema anatambua mchango wa TPA kwa uchumi wa nchi na umuhimu wa bidhaaa zinazoingia nchini kukatiwa Bima.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Bwa.Salim Msangi ameipongeza TPA kwa ufanisi wa kuhudumia shehena.

Chuo cha Bandari kinaendelea kutumia fursa ya ushiriki katika Maonesho ya Wakulima (Nanenane) kukutana na kutoa maelezo ya mafunzo yatolewayo na umuhimu wake,kwa wazazi na wanafunzi wa shule mbalimbali zilipo mjini Dodoma na mikoa ya jirani waliotembelea banda la TPA lililopo viwanja vya Nzuguni

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Said Jafo ametembelea Banda la Bandari ya Mtwara katika kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) ambayo yamehitimishwa rasmi tarehe 08 Agosti, 2025 katika Viwanja vya Ngongo Mkoani Lindi.
Mhe.Dkt. Jafo ameelezea kuvutiwa na utayari wa Bandari ya Mtwara katika kuhudumia shehena mbalimbali ikiwemo mazao ya kilimo kama korosho.
Aidha, ameipongeza Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa kufanya maandalizi mazuri ya maonesho hayo ambapo yamekuwa ya mvuto mkubwa kwa Wananchi.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Dkt. Baraka Mdima ( Wa pili kulia aliyevaa miwani) anahudhuria Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa wa Nchi zisizo na Bahari ( LLDC3) unaofanyika mjini Awaza, Turkmenistan kuanzia Agosti 5 hadi 8 ,2025.
Mkutano huo unalenga kutathmini utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Vienna wa 2014- 2024 na kuweka ajenda mpya ya maendeleo jumuishi kwa miaka kumi ijayo, huku ukijadili changamoto mbalimbali zikiwemo gharama kubwa za usafirishaji, utegemezi wa nchi jirani na miundombinu kwa nchi zisizo na Bahari.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila ametoa pongezi kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw. Plasduce Mbossa na Meneja wa Bandari ya Tanga Bw. Masoud Mrisha kwa utendaji kazi wao uliotukuka hali iliyopelekea kuongezeka kwa ufanisi katika Bandari ya Tanga.
Mhe. Chalamila alitoa pongezi hizo wakati alipotembelea banda la Bandari ya Tanga kwenye Maonesho ya NaneNane Kanda ya Mashariki 2025, yanayofanyika katika Uwanja wa Mwalimu JK Nyerere Mkoani Morogoro.
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya utendaji kazi wa bandari hiyo Mhe. Chalamila alisema kuwa, kuongezeka kwa ufanisi katika Bandari ya Tanga ni pamoja na usimamizi mzuri wa Mkurugenzi Mkuu wa (TPA) pamoja na Meneja wa Bandari hiyo.
Mhe. Chalamila aliongeza kuwa, kuongezeka kwa ufanisi katika bandari hiyo umerahisisha usafirishaji wa shehena ya mazao ya kilimo kutoka Mikoa ya Kanda ya Kaskazini na nchi jirani jambo ambalo ni sifa kwa nchi yetu”.
Aidha Mhe. Chalamila alitoa rai kwa wafanyabiashara nchini kuitumia bandari hiyo kusafirisha mizigo yako kwani usafirishaji kwa njia ya maji hauna mzunguko mrefu na ni salama pia.
Kwa upande wake Afisa Masoko wa Bandari ya Tanga Bw. Ridhiwani Mwasanyagi alimhakikishia Mkuu wa Mkoa huyo bandari ya tanga itaendelea kufanyakazi kwa ufanisi ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwezesha biashara kufanyika kwa ufanisi.
Bandari ya Tanga imekuwa ikisafirisha shehena mbalimbali za mazao ya kilimo kwa uchache kama Mkonge Chai , Kahawa, Macademia hivyo ushiriki wa Bandari ya Tanga kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki 2025, ni kutoa elimu kwa umma na wafanyabiashara wa mazo ya kilimo.