Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inaratibu mpango wa ujenzi wa gati mpya zipatazo 10 ili kuhudumia meli nyingi zaidi kwa wakati mmoja.
Kauli hiyo imetolewa katika kipindi cha maswali na majibu Bungeni leo tarehe 13 Aprili,2026 na Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe.David Kihenzile, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe.Amina Ali Mzee.
Mbunge huyo alitaka kujua mpango wa Serikali wa kuongeza gati katika Bandari ya Dar es salaam ili kuiwezesha kuhudumia meli nyingi zaidi.
Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Tanga ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Meja Mstaafu Hamisi Mkoba imefanya ziara katika Bandari ya Tanga kwa lengo la kukagua hali ya utendajikazi wa bandari hiyo.
Akiongea mara baada kujionea hali ya utendajikazi wa bandari hiyo, Meja Mkoba aliipongeza Menejimenti kwa usimamizi mzuri wa fedha za serikali zilizoletwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika bandari hiyo.
“Mojawapo ya kazi ya kamati hii ni kupitia na kukagua miradi yote ya maendeleo katika Mkoa wetu, hivyo tumeridhishwa na mradi wa maboresho uliofanyika katika bandari hii”. Aliongeza Meja Mstaafu Mkoba.
Awali akitoa taarifa ya mradi wa maboresho yaliyofanyika bandarini hapo,Meneja wa Bandari ya Tanga Bw.Salehe Mbega alisema kuwa, maboresho hayo yamesaidia kutoka kuhudumia meli 110 kwa mwaka hadi meli 450 kwa mwaka.
Kwa upande wa shehena Bw. Mbega alisema kuwa kabla ya maboresho, bandari hiyo ilikuwa inauwezo wa kuhudumia shehena tani 400,000 tu kwa mwaka lakini baada ya maboresho imeweza kuhudumia mpaka shehena tani 1,300,000 kwa mwaka 2024/2025.
Aidha maboresho hayo pia yameongeza fursa za ajira kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga ambapo kwa ajira za kudumu kutoka watumishi 200 mpaka kufikia 344, na kwa upande wa wafanyakazi wa kutwa kutoka 6,000 hadi kufikia 17,000 kwa mwezi.
Katika hatua nyingine Bw. Mbega aliiambia kamati hiyo kwamba, serikali inatarajia kufanya mradi mwingine wa kuongeza gati 3 zenye urefu wa mita 900 ambapo utekelezaji wa awali umeshaanza kufanyika.


Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abed G. Abed tarehe 2 Aprili 2025 amezindua Kamati ya Usalama mahali pa kazi (OSH)kituo cha Bandari ya Dar es Salaam katika hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa Zimamoto na Usalama.
Akizindua kamati hiyo Bw. Abed amesema ni Kamati muhimu kwa kuwa ndio jicho la kwanza la TPA na Menejimenti kwani itasimamia na kuweka uangalizi ili kuzuia vihatarishi vya ajali na majanga na kuimarisha usalama katika shughuli za uendeshaji bandarini.
Amesema kuwa Bandari ya Dar es Salaam ni kinara katika kuhudumia kiwango kikubwa cha shehena, hivyo ni tegemeo kiuchumi ikiwa pia ni sehemu yenye vihatarishi vingi, hivyo usalama na afya katika bandari lazıma upewe kipaumbele.
Naye Meneja zimamoto na Usalama Bw. Mussa Biboze, amesema kuwa kamati hizo zimeundwa kwa kufuata matakwa ya Kanuni na Sheria ya Usalama na afya mahala pa kazi zinazoelekeza waajiri kuhakikisha mahala pa kazi panakuwa na kamati za OSH ili kusimamia usalama wanapokuwa kazini.
Pia alitumia fursa hiyo kuwasihi wajumbe wa Kamati hızo kufanya Kazi kwa bidii ikiwemo kusimamia sheria za usalama na afya Bandarini kwa kuwa uwepo wake katika sehemu za kazi utazuia athari za ajali, majanga na kuimarisha Usalama.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa DOWUTA Bandari ya Dar es Salaam Bw. Mashaka Karume, amesisitiza uwajibikaji katika kutekeleza majukumu na kutenda kazi kiuhalisia ili kuleta matokeo chanya katika kupambana na majanga yanayoweza kuepukika na kuweka mkazo katika kutekeleza majukumu waliyoaminiwa kuyasimamia.


Jumla ya Wafanyakazi 50 wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), wakiongozwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu, Bw. Freddy Liundi, tarehe 30 Machi, 2026 wametembelea Bandari Kavu ya Kwala ili kujionea na kujifunza shughuli mbalimbali za utekelezaji Bandarini hapo.
Ziara hiyo, imelenga haswa kujifunza kuhusu mifumo ya uendeshaji wa bandari, taratibu za usafirishaji wa mizigo, pamoja na fursa zilizopo katika kuboresha biashara ya kimataifa kupitia bandari hiyo.
Bandari hiyo Kavu iliyopo Vigwaza, Kibaha, Mkoa wa Pwani ina hekta 502 (hekta 120 zimesafishwa, ambapo 60 kati ya hizo zimesawazishwa na kujengwa uzio wenye urefu wa Km 2.96, huku hekta 5 zikijengwa kwa sakafu ngumu kwa kiwango cha zege).
Kwa sasa Bandari Kavu ya Kwala ambayo inapokea treni 1 hadi 2 kwa siku ikiwa na makasha ya mizigo huku uwezo wake ikiwa ni kuhifadhi makasha 3,500 kwa wakati mmoja, itasadia kupunguza msongamano wa bandari ya Dar es Salaam kwa 30%.
Bandari hiyo ina uwezo wa kuhudumia wastani wa makasha 823 kwa siku sawa na makasha 300,000 kwa mwaka


Maafisa wa Bandari ya Mtwara wakiongozwa na Meneja wa Bandari Bw. Ferdinand S. Nyathi wamefanya ziara ya kikazi Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) ambapo walipokelewa na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu Bw. Khamis Salum Abdi.
Lengo kuu la ziara hiyo lilikuwa ni kutembelea wateja na wadau wa Bandari ya Mtwara waliopo Visiwani Zanzibar ili kukuza mahusiano yaliyopo, kukusanya maoni na mapendekezo pamoja na kujadiliana kuhusu changamoto zilizopo hususan wakati wa utolewaji wa huduma katika Bandari ya Mtwara.
Katika ziara hiyo, maafisa hao walipata fursa ya kutembelea wadau mbalimbali ikiwemo mwekezaji katika Bandari ya Zanzibar (ZMT) ambaye ni msimamizi mkubwa wa shughuli za uendeshaji wa Bandari hiyo.
Vilevile, walitembelea TP Company ambao ni miongoni mwa wateja wakubwa wa saruji ya Dangote inayosafirishwa kupitia Bandari ya Mtwara na pia walitembelea Bandari ya Fumba.
Ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa kuwa wadau hao waliweza kueleza changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika shughuli zao za kila siku. Maoni na mapendekezo yao yalipokelewa kwa ajili ya kufanyiwa kazi na uboreshwaji huduma. Aidha, maafisa wa Bandari ya Mtwara walipata fursa ya kujifunza mbinu tofauti za kuhudumia shehena, jambo ambalo litasaidia kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.
Kwa ujumla, ziara hiyo inatarajiwa kuimarisha ushirikiano uliopo, kuwa chachu ya maboresho mbalimbali na mabadiliko chanya ya kibiashara katika Bandari ya Mtwara.


EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"