

Viongozi na Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wamejitokeza kwa wingi kutembelea banda la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) katika maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani, yanayofikia kilele chake Juni 25,2025, katika Viwanja vya Mnazi mmoja, Kisiwani Unguja, Zanzibar.
Katika maonesho hayo, TPA imetoa Elimu ya ubaharia kwa Wananchi na Wadau mbalimbali ambao wameipongeza Mamlaka kwa ufanisi mkubwa katika kuhudumia shehena kupitia Bandari zake.
Maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani yana kauli mbiu isemayo “ Bahari yetu, Wajibu Wetu, Fursa Yetu”.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile (Mb), ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA)
kwa namna inavyoendelea kutekeleza wajibu wake wa kimkakati katika maendeleo ya Taifa.
Mhe. Kihenzile ametoa pongezi hizo Juni 19,2025, alipotembelea banda la TPA katika maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Mjini Dodoma.
Mhe. Kihenzile alionesha kuridhishwa na namna Mamlaka hiyo imejipanga kutoa huduma bora kwa wadau wa sekta ya usafirishaji, hususan kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati zinazotegemea bandari za Tanzania kama lango kuu la biashara.
“Ni wazi kuwa TPA ni injini ya uchumi wa Taifa letu. Maendeleo yanayoendelea katika Bandari ya Dar es Salaam, pamoja na juhudi za kuongeza ufanisi katika bandari nyingine kama Tanga, Mtwara na bandari za maziwa, ni hatua muhimu kwa uchumi na maendeleo ya Taifa”. amesema Mhe.Kihenzile.
Aidha, alieleza kufurahishwa na ubunifu wa TPA katika kutumia teknolojia ya kisasa kurahisisha huduma kwa wateja na kuongeza uwazi katika taratibu mbalimbali za bandari.
Mhe. Naibu Waziri alipokewa na maafisa waandamizi wa TPA waliokuwa bandani hapo ambapo walimuhakikishia kuwa Mamlaka itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya usafirishaji na kusimamia kwa weledi mkubwa dhamana waliyopewa ya kusimamia bandari za nchi kwa ufanisi, uwazi na tija kwa maendeleo ya Taifa.
Katika maonesho hayo, TPA imekuwa ikitoa Elimu kuhusu huduma na mifumo mbalimbali inayotumika kutoa huduma bora kwa wateja wake, ikiwa ni pamoja na mifumo ya kidijitali ya kushughulikia mizigo, taarifa za meli, na mawasiliano ya papo kwa papo na wadau.
Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yamehudhuriwa na Taasisi mbalimbali za serikali na zimebeba kaulimbiu isemayo: “Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidijiti ili kuongeza upatikanaji wa Taarifa na kuchagiza Uwajibikaji”.

Wakufunzi na Wanafunzi kutoka Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi “National Institute of Security Studies - (NISS)” cha nchini Nigeria wamefanya ziara katika Bandari ya Dar es Salaam, tarehe 18 Juni, 2025 ili kujifunza namna Bandari inavyofanya kazi.
Ugeni huo uliongozwa na Naibu Kamanda Mkuu wa (NISS) Opoke Ngele na kupokelewa na Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abed G. Abed kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa (TPA) Bw. Plasduce M. Mbossa.