Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw. Plasduce M. Mbossa, tarehe 23 Machi 2026 ameongoza Kikao cha (39) cha Kamati ya Utendaji Baraza Kuu la Wafanyakazi la (TPA) kilichofanyika Mjini Morogoro.
Kikao hicho kimelenga kujadili mapendekezo ya mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Mpango na Bajeti ya kila mwaka inaandaliwa kama mkakati Maalum wa utekelezaji majukumu ya TPA ambayo ni Kumiliki, Kusimamia, Kushirikisha sekta binafsi na Kuendeleza Bandari zote nchini.
Bandari hizo ni pamoja na Bandari Kuu za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara, Bandari ndogo za Kilwa, Lindi, Mafia, Bagamoyo, Pangani na Bandari myingine ndogondogo katika mwambao wa Bahari ya Hindi pamoja na Bandari za Maziwa (Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa).
Kikao cha Kamati ya Utendaji kinakutana kwa siku bili (2) kikifuatiwa na kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi kitakachofanyika tarehe 25 Machi, 2026.


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeipongeza Serikali kwa usimamizi mzuri wa mradi wa ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala, ikieleza kuwa mradi huo ni suluhisho muhimu la changamoto ya msongamano wa malori katika Bandari ya Dar es Salaam na maeneo ya Jiji kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Bandari kavu ya Kwala iliyopo Mkoa wa Pwani, Machi 19, 2026, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Selemani Kakoso( Mb), amesema kukamilika kwa mradi huo kunaongeza ufanisi wa upakuaji na usafirishaji wa Shehena.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa ( Mb) amesema mpango uliopo ni kuiunganisha Bandari Kavu ya Kwala na reli ya SGR na MGR pamoja na bandari nyingine, hatua itakayoongeza ufanisi wa usafirishaji na kupunguza gharama za biashara.
Aliongeza kuwa mradi huo utaenda sambamba na maendeleo ya Eneo Maalumu la Kiuchumi (SEZ) ili kuifanya Kwala kuwa kitovu cha usafirishaji (Regional Logistics Hub).
Aidha, ameihakikishia Kamati kuwa maoni, ushauri na maelekezo yote yaliyotolewa wakati wa ziara hiyo yatafanyiwa kazi kwa lengo la kuongeza zaidi ufanisi wa huduma bandarini na kuimarisha mchango wa sekta ya bandari katika kukuza uchumi wa Taifa.
Naye , Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mha. Dkt. Baraka Mdima kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, amesema mafanikio ya sekta ya bandari yanatokana na ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi, akisisitiza kuwa maboresho yanayoendelea yataongeza ushindani, kuvutia uwekezaji na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.


Bandari za Ziwa Victoria zimefanya kikao cha 61 cha Baraza Dogo la Majadiliano, kilichoongozwa na Mwenyekiti, Bw. Gerald A. Kifaro ambaye ni Kaimu Meneja wa Bandari hizo.
Katika kikao hicho, wajumbe walijadili kwa kina masuala mbalimbali, yakiwemo maendeleo na mafanikio ya Bandari za Ziwa Victoria pamoja na maslahi ya wafanyakazi, kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi na ustawi wa Mamlaka.
Aidha, Baraza lilifanya uchaguzi wa Katibu na Naibu Katibu, ambapo wajumbe walipata fursa ya kuchagua viongozi watakaoendesha shughuli za Baraza hilo kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mwenyekiti Bw. Gerald A. Kifaro aliwasisitiza viongozi waliochaguliwa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu, na kuzingatia kanuni pamoja na taratibu za uendeshaji wa mabaraza.
Kwa ujumla, Bandari za Ziwa Victoria zinaendelea kujikita katika kuimarisha ushirikiano wa ndani, uwajibikaji na maendeleo endelevu kwa manufaa ya Mamlaka na wadau wake.


Serikali imesema imejipanga kuhakikisha miundombinu ya usafirishaji inaendelea kuboreshwa ili kusaidia ukuaji wa biashara na utoaji huduma katika ukanda wa mwambao wa Ziwa Tanganyika.
Akizungumza katika Mkutano wa Kamati ya Uongozi ( Steering Committee) kuhusu mapitio ya miradi ya miundombinu ya Usafiri kwa ajili ya kuimarisha Biashara kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, tarehe 18 Machi,2026 Mjini Kigoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, amesema kuwa maboresho ya bandari, reli pamoja na usafiri wa majini hususan katika Ziwa Tanganyika yataongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na kupunguza gharama za biashara kati ya nchi hizo.
“DRC ni miongoni mwa watumiaji wakubwa wa Bandari za Tanzania, Lengo letu ni kuona ukanda huu unakuwa kitovu cha biashara chenye ushindani mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Hii itasaidia kuvutia uwekezaji na kufungua fursa zaidi za ajira kwa wananchi wetu,” alisema Prof. Kahyarara.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo sekta binafsi ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa wakati.
Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka DRC, Roger Te-Biasu, aliishukuru Tanzania kwa ushirikiano mzuri na kusisitiza kuwa nchi hizo zinaendelea kushirikiana katika miradi ya kimkakati ya miundombinu ili kukuza biashara na uchumi wa kikanda.
Naye Katibu Mtendaji wa wakala wa uwezeshaji wa usafirishaji wa Ushoroba wa kati (CCTTFA), Wakili. Flory Okandju, amewahimiza Wadau wa sekta ya usafirishaji na logistiki kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazojitokeza katika ukanda wa Ziwa Tanganyika ili kuimarisha biashara kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Alibainisha kuwa taasisi hiyo inaendelea kuratibu juhudi za nchi wanachama ikiwemo Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi na DRC kwa lengo la kurahisisha biashara na usafirishaji katika ukanda huo.
Katika majadiliano, kamati imepongeza hatua zilizofikiwa katika bandari, reli, barabara na usafiri wa anga, huku ikibainisha haja ya kuharakisha miradi iliyochelewa hususan upande wa DRC.
Mkutano huo umehitimisha kwa makubaliano ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi, kuendeleza ushirikiano wa karibu, na kuhakikisha fursa zilizopo zinatumika kikamilifu ili kukuza biashara na maendeleo ya kiuchumi kati ya Tanzania na DRC.


Kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa meli nne kubwa za mizigo katika Bandari ya Karema ni fursa kwa wananchi wa mikoa inayopitiwa na Ziwa Tanganyika ya Rukwa, Katavi na Kigoma na kuongeza kipato cha kaya na Taifa.
Ujenzi wa meli hizo ulianza Aprili 2025 na ukitarajiwa kukamilika Julai 2026. Mpaka sasa mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 95 huku meli zote zikiwa majini kwa hatua mbalimbali za uhakiki wa mwisho kuanza kutoa huduma.
Oktoba 2023, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ilipokea maombi kutoka Kampuni ya Gold Voyage Logistics Limited, kampuni tanzu ya Zijin Mining Group Co. Ltd kutoka China ikiomba kukodishwa eneo katika Bandari ya Karema ili kujenga meli hizo.
Hayo yamesemwa tarehe 16 Machi,2026 na Msimamizi Msaidizi wa Bandari ya Karema, Anthony Poyo na wakati wa tukio la kuingizwa majini kwa mara ya kwanza meli ya nne ambapo kukamilika michakato wa vibali ukikamilika zitatoa huduma nchi za DR Congo, Zambia, Burundi na Tanzania mnufaika mkuu kutokana na kuwa na bahari.
Poyo amesema kukamilika kwa meli hizo kutaimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi jirani kama Congo, Burundi na Zambia.
Amebainisha manufaa ya meli hizo kwamba unatarajia kuwa na kichocheo cha usafirishaji wa madini kama ya lithium, shaba na dhahabu kutoka eneo la Manono nchini DRC yanayochimbwa na kampuni hiyo ambapo kupitia Manono, Bandari ya Kalemie hadi Bandari ya Kigoma, Dar es Salaam na Tanga zitatumika kabla ya kusafirisha Kwenda nje ya nchi.


EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"