

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania Bw. Plasduce Mkeli Mbossa anasikitika kutangaza kifo cha RUTH WILFRED MURUVE aliyekuwa Afisa wa Fedha na Uhasibu katika kituo cha Bandari ya Dar es Salaam kilichotokea tarehe 06 Juni 2025 Jijini Dar es Salaam.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi Amani.

Viongozi mbalimbali na Wananchi waliotembelea Banda la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) lililopo katika Viwanja vya Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre Mjini Dodoma, yanakofanyika Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, wameipongeza TPA kwa ufanisi mkubwa katika kuhudumia shehena kupitia Bandari zake na kutunza Mazingira ya bahari na Maziwa.
Miongoni mwa Viongozi hao ni Waziri wa Maji Mhe.Jumaa Aweso (Mb) Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Khamis Hamza Chilo (Mb) Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Anthony Mtaka na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ( TMA) Dkt. Ladislaus Chang’a.
Naye Katibu Mkuu wa Machifu wa Mkoa wa Ruvuma Chifu Akida Wabu Mussa ametoa pongezi kwa Menejimenti ya TPA kwa Ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay ambao kimsingi utakuza biashara katika mikoa ya kusini mwa Tanzania.
Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yamefikia kilele chake Juni 05,2025 ambapo Kitaifa yamefanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete Mjini Dodoma, yakibeba kauli mbiu isemayo “ Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo, Tuwajibike Sasa: Dhibiti Matumizi ya Plastiki.”

Ikiwa katika muendelezo wa kuelekea siku ya Maadhimisho ya Mazingira Duniani, Watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Juni 04,2025, wameungana na wenzao wa Taasisi zingine zilizochini ya Wizara ya Uchukuzi kupanda miti katika Stesheni Kuu ya Samia Suluhu (SGR) Jijini Dodoma

Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Juni 03,2025 imeungana na Taasisi nyingine zilizo chini ya Wizara ya Uchukuzi kushiriki katika zoezi la kufanya usafi eneo la Uwanja wa Ndege wa Dodoma pamoja na maeneo yanayozunguka uwanja huo.
Maadhimisho haya ya kuelekea Siku ya Mazingira Duniani ambayo Kitaifa yatafanyika Mkoani Dodoma chini ya kauli mbiu ya “Mazingira yetu na Tanzania ijayo Tuwajibike Sasa,dhibiti matumizi ya Plastiki”yatafikia kilele Juni 05,2025.
TPA ni mdau makini wa utunzaji wa mazingira ya bahari na maziwa katika maeneo yote zilipo Bandari zake.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Dadi Kolimba amewapongeza Watumishi wa Bandari ya Tanga na kuwataka waendelee kufanya kazi kwa bidii ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika uwekezaji mkubwa uliofanyika katika bandari hiyo.
Mhe. Kolimba ametoa pongezi hizo baada ya kutembelea na kukagua banda la Bandari ya Tanga kwenye maonesho ya 12 ya Biashara na Utalii (Tanga Trade Fair) yanayofanyika katika viwanja vya Mwahako kuanzia tarehe 28 Mei hadi 6 Juni 2025.
“Serikali imewekeza kiasi cha Shilingi Billioni 429.1 hivyo endeleeni kuwajibika ipasavyo ili uwekezaji huo uweze kuzaa matunda sambamba na uhudumiaji wa shehena na ukusanyaji wa mapato uzidi kuongezeka”. Alisema Kolimba.
Awali akitoa maelezo kwa Mkuu wa Wilaya huyo, Kaimu Mkuu wa Idara ya Usaidizi wa Biashara Bi. Rose Tandiko kwa niaba ya Meneja wa Bandari ya Tanga, amesema ushiriki wa Bandari ya Tanga katika maonesho hayo ni kutoa elimu kwa umma juu ya faida inayopatikana baada ya mradi wa maboresho ya Bandari kukamilika sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali katika shughuli mbalimbali za kukuza biashara na Utalii za Mkoa huo.
Pia Bi. Tandiko ametoa rai kwa wafanyabiashara kuitumia Bandari ya Tanga kwani imeboresha huduma zake na hakuna msongamano kutokana na utendaji kazi wenye ufanisi na wafanyakazi wenye ari kubwa.
Aidha Bi Tandiko amesema uwekezaji uliofanywa na Serikali ulikuwa na lengo la kuijengea uwezo bandari hiyo ili iweze kuhudumia shehena kutoka tani 750,000 hadi tani 3,000,000 kwa mwaka.
Maonesho ya 12 ya Biashara na Utalii ambayo husimamiwa na Chemba ya Biashara , Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA ) ambapo kauli mbiu mwaka huu ni “Mwonekano wa Wadau Sekta ya Umma na Binafsi Kwenye Uwekezaji, Ukuaji na Uendelevu wa Biashara”.