

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mhe Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 30 Aprili 2025, amefungua rasmi Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Mawakala wa Forodha Afrika Mashariki na Kati unaofanyika Kisiwani Unguja, Zanzibar na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa Kimataifa katika sekta ya forodha ili kuchochea maendeleo ya biashara na uchumi wa dunia.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya wadau kutoka mataifa mbalimbali, Mhe Abdulla amesema Serikali ya Tanzania Bara na Visiwani zimejipanga kuboresha zaidi mazingira ya biashara kwa kuimarisha mifumo ya forodha, Miundombinu ya Uchukuzi katika nyanja zote ,kupunguza vikwazo vya kikodi na visivyo vya kikodi sambamba na matumizi ya teknolojia ya kisasa ili kuhakikisha huduma bora na za haraka kwa mustabali mpana wa Uchumi wa Tanzania na nchi jirani zinazotumia bandari za Tanzania.
Katika kusisitiza dhamira njema ya Serikali, amesema, Tanzania Bara na Zanzibar, zimewekeza katika miundombinu ya kisasa kama vile bandari, reli na barabara ili kuhakikisha ufanisi wa huduma za forodha na usafirishaji wa shehena.
Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa, amesema Tanzania inaendelea kuimarisha miundombinu ya uchukuzi ili kuifanya nchi kuwa kitovu cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Naye Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt Khalid Salum Mohammed, amebainisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatekeleza mikakati ya kuimarisha bandari na mifumo ya forodha visiwani humo kwa lengo la kuifanya Zanzibar kuwa lango muhimu la biashara za kimataifa.
Awali Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Mawakala wa Ushuru na Forodha (FIATA) Bw. Turgut Erkeskin amesifu juhudi zinazofanywa na Tanzania Bara na Zanzibar katika kuboresha sekta ya forodha.

Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA) tunawatakia Watanzania wote heri ya siku ya Wafanyakazi Duniani- Mei Mosi.

Naibu Waziri wa Biashara Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Tang Wenhon Aprili 28,2025 amefanya ziara katika Bandari ya Dar es Salaam ili kutazama maeneo ambayo nchi yake inakusudia kutoa ushirikiano utakaosaidia ukuaji wa sekta ya Uchukuzi kupitia mpango kazi wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).

Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imeahidi kuendeleza ushirikiano utakaochangia kuimarika na kuukua kwa sekta ya Uchukuzi baina yake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususani bandari na reli kupitia mpango kazi wa FOCAC.
Hayo yamejiri katika kikao baina ya Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa na Naibu Waziri wa Biashara wa China Mhe.Tang Wenhong pamoja na ujumbe wake, makao makuu ya TPA Jijini Dar es Salaam, tarehe 27 Aprili 2025.
Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na China katika sekta ya usafirishaji na biashara hasa kupitia maboresho ya miundombinu ya bandari, Reli ya TAZARA na Ujenzi wa Reli ya kisasa ya SGR.
Katika mkutano huo, viongozi hao walijadili mikakati ya kuharakisha utiaji saini wa Mikataba ya miradi ya maboresho na ukarabati wa Reli ya TAZARA, kuongeza matumizi ya bandari katika kusafirisha shehena, ambapo Naibu Waziri wa Biashara wa China Mhe. Wenhong, amesisitiza dhamira ya serikali yao kuendelea kuwekeza nchini Tanzania, huku akieleza kuwa maendeleo yaliyofanyika kwenye bandari, Ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR unaoendelea, na ukarabati wa reli ya TAZARA utakaofanyika, vitakuwa kichocheo kikubwa cha biashara na mahusiano ya kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania Mhe. Prof. Mbarawa, ameeleza kuwa ushirikiano uliopo baina ya Nchi hizi mbili ni muhimu kwa uchumi wa Taifa na unafungua fursa zaidi kwa wafanyabiashara wa ndani na wa kanda nzima ya Afrika Mashariki.
Mkutano huo umemalizika kwa pande zote mbili kuahidi kuimarisha zaidi urafiki na ushirikiano wa kimaendeleo. Katika Mkutano huo Waziri wa Uchukuzi aliambatana na baadhi ya Viongozi na watumishi kutoka TPA, TAZARA na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.