Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema mradi wa ujenzi wa matanki ya kupokea na kusambaza mafuta ni hatua ya kimkakati ya kuimarisha Tanzania kama kitovu cha biashara na uwekezaji kikanda na kimataifa.
Rais Dkt.Samia amesema hayo wakati alipoweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa matanki ya kupokea na kusambaza mafuta Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Mhe.Rais ameitaka Wizara ya Uchukuzi kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vya Kimataifa ili kukidhi hitaji la ushindani wa soko la Dunia.
Katika hotuba yake ya kumkaribisha Mhe. Rais,Waziri wa Uchukuzi Mhe.Prof .Makame Mbarawa amesema huu ni mradi utakaoongeza uwezo wa bandari katika kuhudumia meli za mafuta na kuifanya Tanzania kuaminika na wadau wa sekta ya usafirishaji wa ndani na Kimataifa.
Katika salamu zake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw.Plasduce Mkeli Mbossa amesema siku ya leo inashuhudia jitihada za dhati za Mhe.Rais Samia Suluhu za kuendeleza kuimarisha uwezo na tija za Bandari ya Dar es Salaam kupitia ujenzi wa mradi matanki ya kuhifadhi na kusambaza mafuta.
Akizungumzia faida za mradi huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 41, Bw.Mbossa amesema utaongeza ufanisi na kupunguza muda wa meli kusubiri kutoka siku 22 mpaka 7.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 3 Machi 2026 ameweka jiwe la msingi la mradi mkubwa wa ujenzi wa Matanki ya Kupokea na Kusambaza Mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mradi huo wa usanifu na ujenzi wa matanki (Tanks Farm) unatekelezwa na wakandarasi wabia ambao ni China Railway Major Bridge Engineering Group Co. Ltd (CRMBEG) na Wuhuan Engineering Co. Ltd kwa gharama ya shilingi bilioni 678.6 ikijumuisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Aidha, Serikali ya Awamu ya Sita kupitia TPA iliingia mkataba wa usimamizi wa mradi kwa kipindi cha miezi 24 na mshauri elekezi Khatib and Alami Consulting Engineering Offshore S.A.L kwa kushirikiana na Projmors na Anova Consult Company Ltd, kwa thamani ya shilingi bilioni 23.2. Hivyo, kufanya jumla ya thamani ya mradi kufikia shilingi bilioni 701.8.
Mradi huu unatarajiwa kuongeza ufanisi wa upokeaji na usambazaji wa mafuta nchini, kupunguza muda wa meli kusubiri bandarini, kupunguza gharama za ucheleweshaji (demurrage) na kuimarisha nafasi ya Bandari ya Dar es Salaam kama kitovu cha biashara ya mafuta katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Hatua hii inaendelea kuonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha miundombinu ya kimkakati kwa ajili ya kukuza uchumi wa taifa na kuongeza ushindani wa bandari za Tanzania kimataifa


.
Serikali imesema mpango wake ni kuhakikisha nchi zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam zinaunganishwa na reli ya kisasa ya SGR ili kurahisisha shughuli za Uchukuzi wa shehena kutoka bandarini.
Kauli hiyo imetolewa tarehe 25 Februari,2026 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof.Godius Kahyarara katika kikao kilichokutanisha ujumbe wa Gavana wa Jimbo la Manyema kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo( DRC) na Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) jijini Dar es Salaam.
Prof.Kahyarara amesema Serikali iko makini na mradi wa ujenzi wa reli hiyo na mpaka kufikia 2029 itakuwa imefika mkoa wa Kigoma.
Katika salamu zake Gavana wa Jimbo la Maniema Mhe.Moïse Mussa Kabwankubi aliyeambatana na wafanyabiashara kutoka nchini DRC,alisema shehena kubwa kutoka jimbo hilo inapitia katika Bandari za Tanzania na lengo la ujio wake ni kuangalia shughulia za uchukuzi wa shehena baina ya nchi hizi mbili.
Katika salamu zake Balozi wa Tanzania nchini DRC Mhe.Balozi Said Juma Mshana,alisema ni jambo la kujivunia kwamba Maraisi wa nchi zote mbili wameendelea kudumisha udugu baina ya nchi hizi unaochochea ukuaji wa biashara na sekta ya uchukuzi kwa ujumla.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA,Mkurugenzi wa Mipango, Ubora na Vihatarishi Dkt. Boniphace Nobeji,alisema shehena ya DRC inayopita Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuongezeka na ndio maana ujenzi wa Bandari za kimkakati unafanyika ili kuhudumia mzigo wa nchi hiyo kwa urahisi,zikiwemo Bandari za Kigoma,Karema na Dar es Salaam


.
Baraza la Wafanyakazi wa Bandari ya Mtwara limefanya kikao chake cha 39 tarehe 23 Februari, 2026 katika Ukumbi wa Klabu ya Bandari.
Kikao hicho kiliongozwa na Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara, Bw. Mtunze M. Sudi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Baraza hilo ambapo wajumbe walijadili masuala mbalimbali yanayohusu utendaji kazi, ustawi wa wafanyakazi, kuimarisha nidhamu ya kazi pamoja na kuboresha mazingira ya kazi ili kuongeza tija na ufanisi wa Bandari.
Aidha, Baraza hilo lilijadili kwa kina suala la uboreshaji wa miundombinu ya Bandari ambapo imesisitiza umuhimu wa kuimarisha magati, kuboresha maeneo ya kuhifadhia mizigo, kuboresha miundombinu ya TEHAMA kwa ajili ya kurahisisha mifumo ya uendeshaji pamoja na kuboresha barabara za ndani na vifaa vya kushughulikia shehena ili kuongeza kasi na usalama katika utoaji huduma.
Baraza lilielekeza juhudi zaidi zifanyike katika kuvutia uwekezaji na kuimarisha matengenezo endelevu ya miundombinu iliyopo ili Bandari iweze kuhudumia meli na shehena kwa viwango vya Kimataifa.
Baraza lilipongeza juhudi za Menejimenti na wafanyakazi kwa ushirikiano unaoendelea kuleta matokeo chanya katika utoaji wa huduma. Aidha, msisitizo mwingine umetolewa kuhusu umuhimu wa uwajibikaji, mawasiliano ya wazi na mshikamano kazini kama msingi wa mafanikio endelevu.
Mwisho, Baraza limeazimia kuendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa maazimio yote yaliyopitishwa katika kikao hicho ili kuhakikisha yanatekelezwa kwa wakati na kwa ufanisi unaotarajiwa
.
Bandari ya Tanga imeendelea kuwa chaguo sahihi kwa wafanyabiashara na wadau wa usafirishaji nchini baada ya kufanikiwa kupokea meli mbili za MV BBC WASHINGTON na MV ZI- JING- SONG zilizobeba mitambo mizito ya kisasa kwa ajili ya miradi mbalimbali inayoendelea nchini.
Meli hizo zimetia nanga katika bandari hiyo moja ikiwa imebeba mitambo ya kudhibiti umeme katika mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la kwenda Uganda (EACOP) na nyingine ikiwa imebeba mitambo ya kisasa ya kuzalisha umeme mali ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Meneja wa Utekelezaji kutoka kampuni ya “East Africa Logisticts Services “ ambaye ndiye msimamizi wa mitambo hiyo Bw. Steve Miller amesema kuwa, mitambo hiyo 95 imeletwa na meli ya MV BBC WASHINGTON kutoka nchini Singapore na inatarajia kwenda Chongoleani Mkoani Tanga kwa ajili ya kudhibiti umeme katika bomba la mafuta kwenda Uganda la EACOP.
Naye wakala wa meli ya MV ZI-JING- SONG kutoka China Bw. Clinton Kitiku wa kampuni ya “Government Clearing Agent” (GPSA) alisema kuwa, meli hiyo iliyokuwa imebeba mitambo 10 ya kufua umeme na matanki 80 ya kuhifadhi mafuta ambayo ni mali ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) inatajiwa kwenda Mikoa ya Tunduma, Iringa na Mbeya.
Ujio wa meli hizo katika Bandari ya Tanga ni baada ya uboreshaji wa miundombinu na uwepo wa vitendea kazi vya kisasa kuweza kuhudumia shehena na mizigo mizito “Heavy lifting” imekuwa kivutio kwa wadau wa usafirishaji kutumia na kuiamini bandari hiyo katika utoaji wa huduma bora

.
EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"