Wajumbe wapya wa Chama cha Wafanyakazi wa Shughuli za Meli na Bandari (DOWUTA) tawi la Dar es Salaam wameaswa kutumia fursa waliyoipata kwa kufanya kazi kwa weledi ili matarajio ya wanaowawakilisha kuweza kufikiwa kwa ufanisi.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abed G. Abed wakati akifungua Baraza la Majadiliano (JIC) la Bandari ya Dar es Salaam linalofanyika mjini Bagamoyo Mkoa wa Pwani.
Amesema kuwa dhamana waliyoipata wanategemewa kwa kiasi kikubwa na Wafanyakazi na pia kama watunga sera au wapitishaji wa mikakati wa mambo yote ya Bandari, hawana budi kujitoa na kufanya kazi kwa uaminifu wa hali ya juu ili matarajio ya wale wanaowawakilisha yaweze kufikiwa.
Aidha Bw. Abed amewapongeza wajumbe hao wa Baraza kwa kuchaguiwa kuwa wawakilishi wa Wafanyakazi na kuwasihi kuwa tayari kujifunza kwa waliowatangulia na kutumia nafasi waliyoipata kuendeleza Taasisi ya TPA.
Pamoja na mambo mengine Baraza hilo limefanya uchaguzi mdogo na kuteua makatibu wapya badala ya Walioshika nyadhifa hizo kujiuzuru ambapo Katibu amechaguliwa Bi.Moni Msemo na Katibu Msaidizi ni Bw. Nasibu F. Wallase.
Waliojiuzuru ni pamoja na aliyekuwa Katibu Bw.Agripa Mjema na katibu Msaidizi Bw. Egidius K. Glegory wote kwa sababu za kiutumishi.
Baraza la Majadiliano (JIC) la Kituo cha Bandari ya Dar es Salaam limelenga kujadili maslahi ya Watumishi na maboresho ya mazingira ya kazi kwa leng kuongeza ufanisi


Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Dkt.Baraka Mdima amewataka Watumishi wapya wa Mamlaka hiyo kuzingatia dira,dhima, kanuni na sheria katika kutekeleza majukumu yao.
Akizungumza wakati akifungua awamu ya pili ya mafunzo kwa Watumishi hao wapya yaliyofanyika Makao Makuu ya TPA jijini Dar es Salaam Machi 16,2026 ,Dkt.Mdima amesema mafunzo hayo yatawapa msingi muhimu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Katika salamu za ukaribisho Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala Bw.Mbarikiwa Masinga amewaambia Watumishi hao kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha kujua vyema malengo na maono ya Mamlaka jambo litakalowawezesha kufanyakazi kwa weledi.


Baraza la Wafanyakazi kituo cha Makao Makuu (HQ) limefanya Kikao chake cha thelathini na tisa (39) mjini Bagamoyo Mkoa wa Pwani.
Baraza hilo limelenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa malengo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa kipindi cha nusu mwaka cha (Julai - Desemba,2025) pamoja na kupokea na kujadili mapendekezo ya Mpango wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027.
Pamoja na mambo mengine Baraza hilo limefanya Uchaguzi wa wajumbe wa kamati ya Utendaji ya Baraza la Uchumi wa tawi la Makao Makuu ambapo washindi katika uchaguzi huo ni Bw. Nassour A. khalifa, Bw. Erick V. Hatia, Bi. Lilian Nicolaus Bhoke na Bi Aziza J. Abdulrahmnan.
Aidha Kati ya hao wawili wameteliwa kuwa Wajumbe wa Baraza kuu la Uchumi la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ((TPA) ambao ni Bi. Aziza J. Abdulrahman na Bw. Nassor A. Khalifa.
Baraza hilo limeongozwa na Mkurugenzi wa Huduma za Tehama Bw. Abdulatif A. Minhajj kwa niaba ya Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Dkt. Baraka R. Mdima


Baraza Dogo la Majadiliano la Bandari ya Mtwara limefanya kikao chake cha 73 tarehe 13 Machi, 2026, kilichoongozwa na Mwenyekiti wake Bw. Ferdinand S. Nyathi ambaye pia ni Meneja wa Bandari ya Mtwara.
Katika kikao hicho, wajumbe walipata fursa ya kujadili na kubainisha mafanikio na mwelekeo chanya unaoendelea kuonekana katika maendeleo ya Bandari ya Mtwara.
Katika majadiliano hayo imeelezwa kuwa, maboresho ya miundombinu ya Bandari yanaendelea kutekelezwa kwa lengo la kuongeza ufanisi wa shughuli za upakiaji na upakuaji wa mizigo. Maboresho hayo yanahusisha ukarabati wa maeneo ya gati, uboreshaji wa maeneo ya kuhifadhia mizigo pamoja na miundombinu ya barabara za ndani ya Bandari, jambo linalorahisisha upitishaji wa magari na mizigo.
Aidha, imeelezwa kuwa kuna ongezeko la matumizi ya Bandari ya Mtwara katika kuhudumia mizigo ya ndani na ya nchi jirani. Hali hii inaonesha kuimarika kwa uwezo wa Bandari katika ushindani wa kimasoko ambapo imeongeza mchango wake katika kukuza biashara na uchumi wa Ukanda wa Kusini mwa Tanzania pamoja na nchi jirani.
Vievile, imeelezwa kuwa juhudi zinaendelea kufanyika katika kuimarisha miundombinu ya TEHAMA ndani ya Bandari ili kuboresha usimamizi wa shughuli za kila siku. Mifumo bora ya kidijitali inasaidia kuongeza uwazi, kupunguza muda wa kuhudumia wateja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Hata hivyo, imebainishwa kuwa kumekuwepo na ushirikiano mzuri kati ya Bandari ya Mtwara na wadau mbalimbali wa sekta ya uchukuzi na biashara. Ushirikiano huu unasaidia kubaini changamoto kwa haraka na kuzifanyia kazi ikiwemo kuweka mikakati ya kuboresha huduma na miundombinu ya Bandari.
Kwa ujumla, kikao kimebainisha kuwa maboresho yanayoendelea katika miundombinu na usimamizi wa Bandari ya Mtwara yanaendelea kuongeza ufanisi wa huduma, kuvutia wateja zaidi na kuimarisha nafasi ya Bandari kama lango kuu na muhimu la biashara katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania na nchi jirani.


Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeipongeza Serikali kwa mabadiliko makubwa ya miundombinu yaliyofanyika katika Bandari ya Tanga na kuleta tija na ufanisi mkubwa katika kuhudumia Shehena.
Pongezi hizo zimetolewa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Prof. Joyce Ndalichako ( Mb) tarehe 13 Machi 2026, baada ya Kamati kutembelea na kukagua mradi wa maboresho wa Bandari ya Tanga.
“ Tunaipongeza sana Serikali kwa kazi kubwa na kiwango kikubwa cha mabadiliko kilichofanyika. Tumeona hakuna kuchelewa wala kukwama kwa huduma ya shehena, hakika mafanikio ni makubwa na mapato yameongezeka sana.” Amesema Mhe. Prof. Ndalichako.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile( Mb) ameishukuru Kamati kwa ziara yao iliyowawezesha kuona kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya sita katika maboresho makubwa ya miundombinu kwenye Bandari ya Tanga huku akiihakikishia kamati hiyo kuwa maoni, ushauri na maelekezo waliyoyatoa yatafanyiwa kazi.
Naye Mkurugenzi wa Mipango, ubora na vihatarishi Dkt. Boniphace Nobeji, akizungumza mbele ya Kamati hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA
amesema, TPA inathamini ushirikiano inaoupata kutoka Serikalini unaopelekea kutekeleza mipango yake inayolenga kuboresha miundombinu na kuleta tija katika Bandari zote nchini.
Mapema akisoma taarifa ya maboresho ya Bandari ya Tanga kwa kamati, Meneja wa Bandari ya Tanga Bw. Salehe Mbega, amesema maboresho ya miundombinu yaliyofanyika katika Bandari ya Tanga yameleta tija na ufanisi mkubwa katika kuhudumia Shehena Bandarini hapo na hivyo kuchagiza ongezeko la makusanyo ya mapato ya Nchi.
Bw. Mbega ameieleza Kamati hiyo kuwa mipango iliyopo sasa ni kujenga gati mpya tatu za mita 900 , kwa kuanza na gati mpya moja ya mita 300 ili kuendelea kuongeza ufanisi wa utoaji huduma katika Bandari hiyo.


EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"