Msafara wa viongozi mbalimbali wanaosoma katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), Machi 12, 2026 wametembelea Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa ajili ya kujifunza shughuli za kibandari.
Wakiongozwa na Mkurugenzi wa Mafunzo wa Chuo hicho, Dkt. Osward Masebu wanafunzi hao ambao ni vingozi wa kada mbalimbali walipata fursa ya kuelezwa kwa kina shughuli za utekelezaji za kibandari na Dkt Boniface Nobeji ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mbossa ambaye naye ni miongoni mwa wanafunzi hao.
Naye Mkurugenzi wa Mafunzo wa Chuo hicho, Dkt. Osward Masebu amesema kwamba wanaishukuru TPA kwa mapokezi mazuri na kuwapa maelezo ya kina kuhusu shughuli za Mamlaka


Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, Machi 10, 2026, amekagua miundombinu na utendaji kazi wa Bandari ya Kasanga iliyopo Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani humo.
TPA ilifanya upanuzi wa bandari ya Kasanga mwaka 2019 kwa kuongeza urefu wa gati kutoka mita 20 hadi 120 kwa kina cha mita 14 pamoja na ujenzi wa nyumba za wafanyakazi na jengo la kuhudumia abiria 200 kwa wakati mmoja kwa gharama ya shilingi bilioni 4.7. Pia kumejengwa maghala mawili ya kuhifadhi mizigo yenye uwezo wa kuhifadhi tani 2,500 kila moja.
Katika kipindi cha Julai 2023 hadi Desemba 2025, bandari hiyo imehudumia jumla ya tani 3,418 za mizigo, abiria 3,648, meli 11 pamoja na maboti 337. Miongoni mwa mizigo inayohudumiwa katika bandari hiyo ni saruji, makaa ya mawe pamoja na mazao ya chakula kama mahindi, mchele na unga wa sembe.
Bandari hiyo ni miongoni mwa miundombinu ya kimkakati inayochochea shughuli za usafirishaji na biashara katika ukanda wa Ziwa Tanganyika na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Rukwa na maeneo jirani.
Wanawake wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wameungana na wanawake wengine kutoka taasisi mbalimbali kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Mburahati, Wilaya ya Ubungo Jijini Dar es Salaam.
Maadhimisho ya mwaka huu yameongozwa na kaulimbiu isemayo “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi Kufikia Dira ya Maendeleo 2050.” Kaulimbiu hiyo inalenga kuhimiza jamii kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata haki sawa na fursa katika nyanja zote za maendeleo.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert John Chalamila, ambaye alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwawezesha wanawake kiuchumi na kijamii ili waweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mhe. Chalamila alieleza kuwa wanawake wana mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi, hivyo ni muhimu kuendelea kuondoa vikwazo vinavyowazuia kupata haki na fursa sawa katika elimu, ajira na uongozi.
Wanawake wa TPA walishiriki katika shughuli mbalimbali za maadhimisho hayo ikiwemo maandamano, maonesho na ujumbe wa kuhamasisha jamii kutambua na kuheshimu haki za wanawake na wasichana.
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 8 Machi, yakilenga kutambua mchango wa wanawake katika maendeleo ya jamii pamoja na kuhimiza usawa wa kijinsia.



Watumishi wanawake wa Bandari za Ziwa Victoria wakiongozwa na Meneja wa Bandari, Bi. Rosemary Ndesamburo, wameungana na wanawake wengine wa Mkoa wa Mwanza kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Nyamhongolo, Wilaya ya Ilemela, Mkoa wa Mwanza.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika kwa kauli mbiu ya “Haki ya Wanawake na Wasichana ni Msingi wa Maendeleo Jumuishi kufikia Dira ya 2050” yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali, ambapo mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe. Mkuu wa Mkoa aliwahimiza wanawake kuendelea kujijenga kiuchumi na kijamii kwa kufanya kazi kwa bidii, kujithamini na kujiandaa vyema kwa maisha yao ya baadaye, hususani kipindi cha uzeeni. Aidha, aliwasisitiza wanawake kuendelea kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira, ikiwemo kupanda miti na kutunza rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wao, watumishi wanawake wa Bandari za Ziwa Victoria walieleza kuwa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ni fursa muhimu ya kuendelea kuhamasisha usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake na mchango wao katika maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Menejimenti ya Bandari za Ziwa Victoria inaendelea kuthamini na kuunga mkono juhudi za kuwawezesha wanawake katika maeneo ya kazi na katika jamii, kwa kutambua kuwa wanawake ni nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo endelevu ya Taifa


Katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka 2026 Watumishi Wanawake wa Bandari ya Tanga waliungana na Wafanyakazi Wanawake wa kutwa wa bandari hiyo kufanya matendo ya huruma.
Wanawake hao, walitoa msaada wa Mashine za kusaidia upumuaji aina ya “C- PAP Bubble Neonates, Oxygen Flowmeter” pamoja na vifaa mbalimbali katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, Bombo vyenye thamani ya Shilingi Milioni 5.
Akizungumza wakati wa kukabidhi Mashine hizo, Afisa Mkuu Rasilimali Watu wa Bandari hiyo, Bi. Sharifa Nuhu alisema, wamekuwa na utaratibu wa kila mwaka kutumia siku hiyo kufanya matendo ya huruma kwa jamii na mwaka huu wasaidie Hospital ya Rufaa ya Mkoa, Bombo.
“ Mwaka huu tumeona tuunge mkono juhudi za Serikali katika kuboresha afya za watoto, hivyo tukaona tutoe msaada wa Mashine hizo katika wodi ya watoto wachanga katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo sababu ndio hospitali kubwa ambayo hata wagonjwa kutoka hospitali za Wilaya hupewa rufaa ya kuja hapa kufanya uchunguzi zaidi wa kitabibu”. Aliongeza Bi. Nuhu.
Awali akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa, Dkt . Abdi Msangi aliwashukuru Watumishi hao kwa msaada walioutoa kwani umetolewa wakati muafaka kutokana na uwepo wa upungufu wa mashine hizo katika wodi ya watoto wachanga wenye matatizo ya upumuaji.
Aidha Daktari Bingwa wa Watoto katika Hospitali hiyo, Dkt. Mohamed Salehe alisema kuwa Mashine hizo zitakuwa msaada mkubwa hospitalini hapo ikizingatiwa kwa sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la watoto wanaozaliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na shida ya upumuaji. Kwa hiyo vifaa hivyo vitaenda kuboresha huduma ya upatikanaji wa huduma katika wodi ya watoto.

”
EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"