

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi ameiagiza Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha Mradi wa Usanifu na Ujenzi wa Bandari mpya wa Mbamba Bay iliyopo Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma unakamikika kwa wakati na kwa ubora.
Akizungumza tarehe 05 Aprili,2025 baada ya kutembelea na kukagua mradi huo mkubwa na wa kimkakati, Mhe. Balozi Nchimbi amesema kukamilika kwa Bandari ya Mbamba Bay, kutaimarisha zaidi Biashara katika ukanda wa mikoa ya kusini na nchi jirani za Malawi na Msumbuji.“
“ Mradi huu ni muhimu na faraja kubwa kwa wana Nyasa na unasubiriwa kukamilika kwake. TPA hakikisheni mnausimamia kwa nguvu zenu zote kwani ni Jambo Jema kwa maendeleo ya nchi yetu.” Amesema Mhe. Balozi Nchimbi.
Mhe.Balozi Nchimbi pia ameipongeza Menejimenti ya TPA kwa kuusimamia vyema Mradi huo muhimu na wa kimkakati ambao anasema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatoa umuhimu wa pekee katika kukamilika kwake.
Mapema akitoa maelezo ya mradi huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Bw. Plasduce Mbossa, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Dkt. Baraka Mdima, amesema mradi huo utakaojengwa kwa miezi 24, unatarajia kukamilika kwa wakati kwa mujibu wa mkataba.
Amesema ujenzi wa Bandari ukikamilika utafungua biashara kati ya Tanzania na nchi za Zambia, Malawi na Msumbiji na kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar-es-Salaam, kuongeza ufanisi katika Bandari ya Mtwara na kuimarisha kiuchumi ushoroba wa kusini.
Mradi huu unajengwa katika eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 49,700 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 81 ambapo kwa sasa umefikia asilimia 26 na unatarajia kukamilika katika kipindi cha miezi 24.
Jiwe la msingi la usanifu na Ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay, liliwekwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Septemba 25, 2024.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi ( Kulia) akimkabidhi Tuzo ya shukurani kwa kutambua mchango wa TPA kufanikisha Mkutano Mkuu Maalum wa mwaka wa Jukwaa la Wahariri ( TEF) kwa Kaimu Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA), Bw. Leonard Magomba( wa pili kushoto) ambaye alipokea kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Bw. Plasduce Mbossa, wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo Mkuu Maalum wa mwaka wa TEF, tarehe 4 Aprili,2025 Mjini Songea Mkoani Ruvuma.
Mhe. Balozi Dkt. Nchimbi alikuwa Mgeni Rasmi katika Mkutano Mkuu huo Maalumu ambapo amesisitiza umuhimu wa vyombo vya Habari katika kukuza maendeleo ya nchi. Pamoja na mambo mengine, wanahabari hao waliutumia Mkutano Mkuu huo Maalum kufanya uchaguzi wa uongozi wao mpya.

Serikali ya Tanzania na ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wamekamilisha majadiliano ya kukabidhiana Ardhi zilizotengwa kwa ajili ya uendelezaji wa miundombinu ya Bandari Kavu katika nchi hizo ikiwa ni miongoni mwa utekelezaji wa mkakati wa kukuza biashara.
Akizungumza katika tukio hilo mjini LUBUMBASHI nchini DRC, katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara amesema kuwa hatua hiyo ni matokeo muhimu katika kutekeleza makubaliano ya uendelezaji wa miundombinu ya Uchukuzi yalisainiwa mwaka 2022 ili kukuza biashara baina ya nchi hizo mbili pamoja na kuboresha mazingira ya usafirishaji mizigo kupitia Bandari ya Dar es Salaam.
Baada ya kukamilishwa kwa mazungumzo hayo, Pande zote mbili zinaendelea na ukamilishaji wa taratibu za umilikishwaji wa Ardhi kwa ajili ya ujenzi na uendelezaji wa Bandari kavu ambapo kwa DRC, Tanzania itapewa maeneo ya Kasumbalesa, Kasenga na Kalemie huku kwa upande wa Tanzania, DRC itapewa maeneo ya Bandari kavu katika eneo la Kwala Mkoani Pwani na Katosho Mkoani Kigoma.
DRC moja ya masoko yenye wateja wakubwa wanaotumia Bandari ya Dar es Salaam na Tanga kusafirisha mizigo ya aina mbalimbali inayotoka na kuingia nchini DRC.
Tanzania na DRC ni miongoni mwa nchi Saba zilizopo katika ushoroba wa kati (central corridor) ambapo lengo lake kuu ni kurahisisha usafirishaji kwa kuimarisha miundombinu ya barabara, reli, usafiri wa majini pamoja na anga.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeipongeza Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA) kwa usimamizi mzuri wa matumizi ya Fedha za Maboresho yanayoendelea kufanyika kupitia mradi wa maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam (DMGP)
Akizugumza tarehe 30 Machi 2025, mara baada ya kumaliza ziara ya kukagua na kutembelea mradi wa maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam, Mwenyekiti wa PAC , Mhe.Naghenjwa Kaboyoka (Mb) amesema kamati yake imejiridhisha na usimamizi mzuri wa Mradi huo na Fedha za Umma zimetumika vyema na kufikia malengo yakiyokusudiwa.
“ Kamati imejiridhisha na kazi nzuri iliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam, kazi yetu kubwa ni kuangalia Kama Fedha za Umma zimetumika vizuri kwa manufaa ya nchi yetu na katika hili Kamati inampongeza sana Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti ya TPA na Wafanyakazi wote kwa kazi nzuri iliyofanyika hapa.’ Amesema Mhe. Kaboyoka.
Akijibu hoja za Wajumbe wa Kamati hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPA, Mhe. Balozi na IGP Mstaafu Ernest Mangu, ameishukuru Kamati kwa kufanya ziara yao iliyowawezesha kuona hatua iliyofikiwa na thamani ya mradi wa DMGP, huku akiihakikishia kamati hiyo kuwa maelekezo, maoni na ushauri wao utafanyiwa kazi.
Mapema akisoma taarifa ya mradi wa maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam (DMGP) mbele ya kamati kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Bw. Plasduce Mbossa, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Dkt. Baraka Mdima, amesema hadi sasa kukamilika kwa utekelezaji wa mradi katika baadhi ya maeneo kumeleta manufaa mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia Meli kubwa zenye kubeba makasha hadi 8,000, kuongezeka uwezo wa kuhudumia shehena kutoka tani milioni 16 hadi tani milioni 28 kwa sasa na kuongeza uwezo wa kiushindani kati ya Bandari ya Dar es Salaam na Bandari nyingine.
Mradi wa maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam (DMGP) unagharimu Shilingi Trilioni 1.118 ambazo ni Fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia, Fedha za msaada kutoka kwa Wafadhili na mapato ya ndani ya TPA.
Mradi huu umehusisha kuimarisha Gati na 1-7 na kuongeza kina kutoka mita 8 hadi mita 14.5 na kujenga Gati maalum ( RoRo Berth) la kuhudumia meli za magari, kuongeza kina na Upana wa lango la kuingilia Meli na eneo la kugeuzia Meli , kuimarisha Gati na 8-11 na kuongeza kina kutoka mita 12 hadi kufikia kina cha mita 14.5, kuboresha mtandao wa Reli ndani ya Bandari na kusimika Mfumo wa Umeme Bandarini.
- TPA YASHIRIKI EAST AFRICA CARGO CONNECT SUMMIT JIJINI DAR ES SALAAM
- BANDARI YA MTWARA YAONGEZA KWA UFANISI WA KUHUDUMIA SHEHENA MCHANGANYIKO IKIWEMO ZA KEMIKALI
- KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UWEKEWZAJI WA MITAJI YA UMMA (PIC) YAKAGUA MABORESHO YA UPANUZI WA BANDARI YA MWANZA KASKAZINI
- BARAZA KUU LA WAFANYAKAZI TPA KATIKA KIKAO MJINI BAGAMOYO