Ufanisi wa uhudumiaji wa shehena mbalimbali katika Bandari za TPA umeongezeka, huku bandari ya Dar es Salaam ufanisi wake ukizidi kuimarika na shehena kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 36 kwa mwaka, kasi ambayo haijapata kutokea tangu kuanzishwa kwake.
Akizungumza wakati wa kufungua Mkutano wa 18 wa Tathimini ya Utendaji wa Sekta ya Uchukuzi uliofanyika katika kituo cha mikutano cha kimataifa Arusha (AICC) Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile (Mb) amesema, ufanisi unaoshuhudiwa kulingana na takwimu za shehena zaidi ya Tani Milioni 34 zinazohudumiwa katika Bandari zote nchini za mwambao wa Bahari na Maziwa Makuu, ni matokeo ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema mpango wa mradi mkubwa wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara ujenzi wa Bandari ya Kisiwa Mgao na Bagamoyo unaoendea sambamba na maboresho ya bandari za maziwa, matumizi ya vifaa vya kisasa na mifumo ya kisasa ya TEHAMA, imesaidia kuongezeka kwa shehena inayoingia na kutoka kupitia katika bandari zote nchini.
Katika salamu zake za ukaribisho Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Kahyarara amesema, kasi ya ukuaji wa Bandari si ya kawaida kwani imekuwa ikiongezeka kwa asilimia 36 kwa mwaka.
Aidha amesema ushindani ni muhimu kwa sababu unaleta changamoto ya kufanya vizuri zaidi na kuwekeza zaidi katika Bandari zetu.Sambamba na mkutano huo wa tathimini, Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Uchukuzi zinashiriki kwenye maonesho yanayoambatana na mkutano yanayofanyika katika viwanja vya AICC.


Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mha. Dkt. Baraka Mdima, amepokea Cheti cha Pongezi kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA kutoka Chuo cha Dar es Salaam Maritime Institute (DMI) katika Mahafali ya 21 ya Chuo hicho, tarehe 12 Disemba,2025 Jijini Dar es Salaam.
Cheti hicho kimetolewa na DMI ikiwa ni ishara ya kutambua mchango mkubwa wa TPA katika kutoa nafasi za Mafunzo ya Vitendo (Industrial Practical Training – IPT) kwa wanafunzi wa chuo hicho kwa mwaka wa masomo 2024/2025.
Dkt. Mdima ameishukuru DMI kwa kutambua mchango wa TPA na kusisitiza kuwa Mamlaka itaendelea kushirikiana na Taasisi za elimu katika kukuza ujuzi na uwezo wa wataalamu wa sekta ya uchukuzi na usafirishaji.


Serikali imepanga kuanza ujenzi wa gati 10 mpya katika Bandari ya Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuifanya sekta ya uchukuzi kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa.
Kauli ya Serikali imetolewa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile (Mb), tarehe 11 Disemba 2025, alipomuwakilisha Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, katika hafla ya uzinduzi wa mtambo mpya wa Reach Stacker uliofanyika katika Bandari Kavu ya Zambia Cargo & Logistics Limited, jijini Dar es Salaam.
Amefafanua kuwa ujenzi huo wa gati 10 mpya utaifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa na jumla ya gati 22 zitakazowezesha kuhudumia meli kwa ufanisi na kuongeza uwezo wa upitishaji mizigo.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa matanki 15 ya kuhifadhia na kusambaza mafuta yaliyopo Kigamboni, ujenzi wa Bandari mpya ya Bagamoyo, ujenzi wa gati jipya eneo la Kisiwa Mgao Mkoani Mtwara na bujenzi wa Bandari mpya ya Mbamba Bay.
Aidha, Naibu Waziri Kihenzile ameihakikishia Serikali ya Zambia kuwa Tanzania itaendelea kudumisha ushirikiano wa muda mrefu katika sekta ya uchukuzi na biashara, ushirikiano ambao utanufaisha wananchi wa pande zote mbili za Tanzania na Zambia.


Bandari ya Mtwara imeendelea kupongezwa kwa utendaji kazi wenye ufanisi mkubwa na tija katika kuhudumia shehena mbalimbali za ndani na nje ya Nchi.
Pongezi hizo zimetolewa tarehe 11 Disemba 2025, na Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb.), wakati wa ziara yake ya kutembelea Bandari ya Mtwara.
Mhe. Chongolo ameonesha kuridhishwa na hali nzuri ya miundombinu, mitambo na vitendea kazi vya kisasa, ambavyo vyote ni matokeo ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika kuboresha uwezo wa bandari hiyo.
Kwa upande wake, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Bw. Ferdinand Nyathi, amesema kuwa bandari hiyo inaendelea kuhudumia shehena ya korosho kwa ufanisi mkubwa pamoja na shehena nyingine mbalimbali. Ameongeza kuwa muda wa wastani wa kuhudumia meli na shehena umepungua kutoka siku 7 hadi siku 4, hatua inayoonesha maboresho makubwa ya kiutendaji.


Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Disemba 11 ,2025, imeshiriki kikao cha Wadau kuhusu uthibitishaji wa Tozo za huduma za Kibandari, kilichoandaliwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC).
Kikao hicho cha siku moja kimefanyika Jijini Dar es Salaam, kikiwa na lengo la kukusanya maoni kutoka kwa umma na wadau wa bandari kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya tozo za huduma za Kibandari.


EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"