

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw. Plasduce Mbossa, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono yake thabiti na uongozi wake mahiri ambao umeifanya sekta ya bandari kuwa kiungo muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Bw. Mbossa ametoa pongezi hizo leo tarehe 24 Februari,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma, kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Mamlaka katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita.
“ kama mnavyofahamu sekta ya Bandari imekuwa na mabadiliko makubwa tangu Serikali ya awamu ya sita iingie madarakani na sababu kubwa ni uongozi thabiti na maono ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kuiimarisha sekta hii na katika hili tunamshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais.” Amesema Bw. Mbossa
Amesema kupitia uongozi dhabiti wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania inaendelea kujiimarisha kama kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“ Tunaishukuru Serikali kwani kupitia TPA inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ili kuimarisha miundombinu ya bandari, kuongeza ufanisi wa utoaji huduma, na kuvutia biashara kwa lengo la kukuza uchumi wa taifa.” Amesema Bw. Mbossa.
Amesisitiza kuwa TPA itaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kwa kuhakikisha uwekezaji unaochochea maendeleo endelevu katika sekta ya bandari unatekelezwa kwa tija na ufanisi wa hali ya juu.
Vilevile, Bw. Mbossa amesisitiza kuwa TPA itaendelea kuhakikisha bandari zinakuwa lango bora la biashara kwa maendeleo ya Taifa.

Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa kikamkati wa matenki maalum ya kuhifadhi na kusambaza mafuta ( Oil Terminal) na kutoa maelekezo kwa Makandarasi wanaojenga mradi huo ukamilike kwa wakati na kwa ubora.
Akizungumza tarehe 19 Februari,2025 baada ya kutembelea mradi huo unaojengwa katika kata ya Tundwi, wilaya ya Kigamboni Jijini Dar es Salaam, Mhe. Prof. Mbarawa amesema pamoja na kuridhishwa na maendeleo ya mradi huo ni muhimu mradi ukasimamiwa vyema ili ukamilike kwa wakati na kwa ubora kwani kukamilika kwake kutasaidia kuboresha ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam na kupunguza kwa kiwango kikubwa foleni ya Meli za kupakua mafuta.
“ Mara ya mwisho nilipokuja hapa mwezi Septemba mwaka jana mradi huu ulikuwa asilimia 5 tu na sasa umefikia asilimia 14.77. Hakika kazi inaenda vizuri n inaonekana, muhimu ni kwa Makandarasi hawa kuongeza bidii, kufanya kazi kwa ubora na mradi huu ukamilike kwa wakati ,” amesema Mhe. Prof. Mbarawa.
Amesema Serikali imeamua kujenga matenki hayo 15 ya kuhifadhi na kusambaza mafuta yenye ujazo wa mita za ujazo 378,000 ili kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kiwa moja ya Bandari zenye ushindani duniani pia kukabiliana na uhaba wa mafuta unaoweza kutokea.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Dkt. Baraka Mdima, amesema mradi huo unaojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 678.6 kwa sasa umefikia Asilimia 14.77 tangu ulipoanza Agosti 16,2024 na utasimamiwa vyema na kumalizika kwa wakati ndani ya miaka miwili kwa mujibu wa mkataba na kuwa na tija kwa bandari ya Dar es Salaam na Serikali kwa ujumla katika kukusanya kodi na tozo mbalimbali.
“ Tumepokea maelekezo ya Mheshimiwa Waziri ya kuhimiza utendaji na kimsingi ameridhika na kazi inayofanyika hapa na amehimiza ifanyike kwa bidii na mradi ukamilike kwa wakati, tumepokea maelekezo na tutayatekeleza,” amesema Dkt. Mdima.
Mradi huo wa Matenki 15 ya kuhifadhi na kusambaza mafuta, utahusisha matenki sita ya kuhifadhi mafuta ya do seli, matenki matano ya kuhifadhia mafuta ya petroli, matenki matatu ya kuhifadhia mafuta ya kuendeshea ndege na tenki moja litakuwa la ziada likitumika kupitishia mafuta (Interface tank).

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Serikali ya Uingereza imesema imefurahishwa na juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika uboreshaji wa miundombinu na utoaji wa huduma katika bandari ya Dar es salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea Bandari ya Dar es Salam jana, Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Bw Lord Collins amesema kuwa wakiwa kama sehemu ya wadau wa bandari ya Dar es salaam wanajivunia kuona miundombinu ya bandari imeboreshwa na kwa kiasi kikubwa imeongeza ufanisi mkubwa kiutendaji na pia imeendelea kupiga hatua katika Nyanja ya utoaji huduma bandarini hapo.
“Napenda kuchukau nafasi hii kuipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandaari Tanzania(TPA) pamoja na viongozi wote kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika hapa bandarini,” alisema Bw Collins ambaye aliambatana na Balozi wa Uingereza hapa Tanzania, Bi Marianne Young.
Waziri Collins alisema bandari ya Dar es Salaam ni mfano wa bandari ya kuigwa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki kwa sababu inaunganisha Tanzania na nchi zote ambazo zinaizunguka Tanzania, hivyo maboresho yake yataongeza tija zaidi.
“Najua maboresho haya yanaongeza tija na ajira hasa kwa Watanzania ambao ndiyo wanufaika wa kwanza wa uwekezaji huu, hivyo tunafurahi kuona neema zaidi kwa wananchi wa Tanzania” aliongeza Bw Collins.
Serikali ya Uingereza kupitia shirika lake la misaada la (UK Aid) ni miongoni mwa Wadau wa Maendeleo walifanikisha kuchangia maboresho ya miundombinu mbalimbali katika bandari ya Dar es Salaam kama vile ujenzi wa barabara za ndani, uboreshwaji wa eneo la maegesho pamoja na teknolojia ya mtandao unaosaidia kazi mbalimbali bandarini hapo.
Kwaupande wake Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Bandari Dkt Baraka Mdima amesema kuwa ugeni wa viongozi kutoka serikali ya Uingereza ni fursa kubwa kwa Tanzania katika nyanja ya uhusiano wa kiuchumi kupitia usafirishaji wa mizigo katika bandari ya Dar es salaam.
Naye Kaimu Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Dkt Baraka Mdima alisema ugeni huo ni chachu kubwa kwa maendeleo yanayoonekana kwenye bandari hiyo.
“Mchango wa Serikali ya Uingereza ni mkubwa sana na hatuna budi kuwashukuru kwani hivi sasa sasa tunapata meli nyingi ambazo hapo awali zilikuwa hazifiki na sambamba na hilo hata idadi ya shehena pia imeongezeka na kuchangia ongezeko la pato la la taifa” alisema Dkt Mdima.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Bw Mbelwa Kairuki ubalozi unafanya uhamasishaji mkubwa mkubwa kwa wafanyabishara nchini Uingereza kuja kufanya bishara hapa Tanzania.
Aliiomba Uingereza kufungua zaidi milango kwa watazania wanaopenda Kwenda kuwekeza zaidi nchini uingereza.
MWISHO.

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeibuka Mshindi wa Tatu katika Kundi la Taasisi Umma zinazozingatia na kufuata Miongozo na Kanuni za Mamlaka ya Serikali Mtandao katika uendeshaji na usimamizi wa mifumo ya TEHAMA katika shughuli zake.
TPA imepata jumla ya asilimia 91.11 katika Tathmini ya uzingatiaji wa Kanuni na Miongozo inayotolewa na e-GA katika uendeshaji Serikali Mtandao.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora Mhe. George Boniface Simbachawene amefunga Kongamano la 5 la Mwaka la Serikali Mtandao, tarehe 13 Februari, 2025 jijini Arusha na kuwaelekeza Viongozi na watumishi wa Umma kuzingatia na kutekeleza maazimio 6 ya Kikao hicho ipasavyo.
Mhe. Simbachawene amehimiza umuhimu wa kutekeleza maazimio hayo ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuboresha huduma za Serikali kwa wananchi wake kwa mifumo ya kidigitali.
Kongamano hilo lililokuwa na Kauli Mbiu “ Huduma za Serikali Mtandao na ubunifu wa Utoaji Huduma za Mifumo ya TEHAMA kwa wananchi kwa ufanisi” limejadili jitihada za e-GA katika kujenga Serikali mtandao.
Masuala mengine yaliyojiri katika kikao hicho ni kubainisha fursa na changamoto za utekelezaji Serikali Mtandao pamoja na mbinu bora za kufanikisha na kuendesha Serikali Mtandao. Kongamano la 5 la Mwaka la Serikali Mtandao limehudhuriwa na washiriki zaidi ya 1,000 kutoka Seriikali Kuu, Serikali za Mitaa, Taasisi na Mamlaka za umma, Sekta Binafsi na Wataalamu kutoka nje ya Nchi.

Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abed Gallus Abed amekutana na Wadau na watumiaji mbalimbali wa Bandari hiyo katika kikao kilicholenga kusikiliza na kutatua changamoto zinazohusiana na shughuli za kibandari.
Kikao hicho cha siku moja kimefanyika Februari 14,2025 katika Ukumbi wa mikutano wa Bandari ya Dar es Salaam, kimehitimishwa kwa Bw.Gallus kuwataka wadau kushirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoathiri ufanisi wa Bandari pamoja na kuhakikisha maazimio ya kikao hicho yanatekelezwa.