

Baraza la Wafanyakazi la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kituo cha Makao Makuu limefanya kikao cha thelathini na saba (37) tarehe 14 Februari, 2025 mjini Bagamoyo, chenye lengo la kupokea taarifa ya utekelezaji wa malengo kwa mwaka wa fedha 2024/2025. kwa kipindi cha nusu mwaka (Julai - Desemba 2024) pamoja na kupokea mapendekezo ya Mpango wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Baraza hilo limeongozwa na Kaimu Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Dkt. Baraka R. Mdima kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Bw.Plasduce M. Mbossa.

Na Leonard Magomba
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Chuo cha Arab Academy for Science Technology and Maritime Transport (AASTMT) cha nchini Misri zimesaini randama ya makubaliano ya kushirikiana katika kutoa mafunzo ya shughuli za kibandari kwa wafanyakazi wa Mamlaka.
Akizungumza muda mfupi mara baada ya kusaini randama ya makubaliano hayo yaliyoshuhudiwa na kundi la kwanza la wafanyakazi 23 waliopata fursa ya kwenda kusomea fani za uhandisi wa baharini na uendeshaji meli katika Chuo hicho, jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mbossa amesema makubaliano hayo ni sehemu ya mpango wa mamlaka wa kuwaendeleza wafanyakazi, kuongeza ufanisi pamoja na kuifanya TPA kuwa sehemu sahihi.
“Makubaliano haya ni kielelezo cha dhamira ya TPA kutaka kuwaendeleza wafanyakazi wake wawe na ujuzi na maarifa stahiki katika uendeshaji na ufanyaji kazi za bandari," alisema, Bw Mbossa.
Alisema kwamba TPA imejipanga kuendeleza uwezo wa wafanyakazi wake katika kutoa huduma maeneo yote muhimu ya ndani ya maji na ardhini. Na hii ni hatua muhimu katika kutanua shughuli zetu za utoaji huduma kwa wateja wanaotumia bandari zetu.”
“Makubaliano haya yatawezesha wafanyakazi wetu kupata mafunzo katika chuo hicho nchini Misri chenye uzoefu wa masuala yanayohusu bandari ili kuwajengea uwezo na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma katika bandari zetu hapa nchini,” amesema Bw Mbossa.
Amesema TPA imeamua kuingia makubaliano na chuo hiki kwa sababu ya uzoefu wake katika kutoa mafunzo yenye ubora wa ngazi za kimataifa.
“Tuliangalia vyuo vingi, lakini tuliamua kuingia makubaliano na chuo hiki cha Misri baada ya kuridhishwa na weledi sambamba na uzoefu wake,”alisema bosi huyo wa TPA na kuongeza kuwa.
“Tumekuwa na mahusiano na chuo hiki kwa muda mrefu ambapo katika miaka ya nyuma tulipeleka manahodha wetu wa meli na wafanyakazi wengine wa idara mbalimbali kupata mafunzo ya kuongeza ufanisi na mafunzo mengine ni ya ulazima katika kuhuisha vyeti vyao,” amesema Mbossa.
Amesema vijana watakaokwenda kupata masomo ya muda mrefu katika chuo hicho kwa sasa ni wale wenye elimu ya kidato cha sita ambao wataongezewa ujuzi na kupata vyeti ili kutoa huduma bora katika bandari mbalimbali hapa nchini. Kwa upande wake, Rais wa Chuo hicho, Prof Ismail Abdelghaffar amesema kwa kusaini makubaliano haya,taasisi hizi mbili zinaanza safari mpya ya pamoja kuelekea kutimizi ndoto na matarajio ya pamoja kitaaluma.
“Nimefurahi sana na nina heshima kubwa kukutana na viongozi wa kipekee wa sekta ya baharini hapa Tanzania,”
“Dira yao, mikakati yao, kazi yao, kujitolea kwao, na imani yao katika kuwekeza katika rasilimali watu ni muhimu sana kwa mustakabali wa sekta hii muhimu ya baharini,” amesema Prof Abdelghaffar.
Ameongeza kuwa chuo chao kitafanya kazi kwa pamoja na TPA katika kukuza rasilimali watu wa baadaye kwa sekta hii.
“Ufanisi na uweledi wa bandari utazidi kuongezeka kwa kuwa na watoa huduma wenye ujuzi na hadhi ya kimataifa,” alisema na kuwa ni muhimu sana katika mahitaji ya soko la ushindani kwa sasa.
TPA imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuongeza ufanisi wa utendaji katika bandari zake ambapo Umoja wa Wafanyabishara nchini Tanzania (UWT) hivi karibuni walitembelea katika bandari ya Dar es Salaam kujionea uwekezaji mkubwa uliofanyika na kuridhishwa na matokeo yake makubwa ya kasi ya kushusha na kupakia mizigo kwa mitambo ya kisasa.
Mwisho.

Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imeendelea kung’ara kwa mara ya tatu mfululizo kwa kutwaa Tuzo ya Mwajiri Bora wa mwaka katika Sekta ya Umma kwa mwaka 2024.
Tuzo hiyo imetolewa Jijini Dar es Salaam na mgeni rasmi, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt Doto Biteko, ambaye alimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Philip Mpango, na kupokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mkeli Mbossa.
“TPA si kwamba tu inafanya vizuri kiuchumi, bali pia imeonyesha kwamba ni mwajiri wa kupigiwa mfano na wengine hapa nchini, amesema Dkt. Biteko na kuongeza kwamba taasisi nyingine kuiga mfano huu.”
TPA pia ilitangazwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kuwa imetwaa Tuzo nyingine nne, ikiwemo Tuzo ya Mwajiri Bora Mzawa (Local Employer Award), ambayo iliiweka Mamlaka hiyo kwenye nafasi ya mshindi wa kwanza.
Aidha, TPA pia ilitwaa Tuzo ya mshindi wa tatu wa Jumla katika Sekta zote. Tuzo nyingine ni ya Taasisi zinazofanya vizuri zaidi (Club of Best Performers) na Tuzo ya mwisho ni ya kuwa Mwanachama wa ATE kwa muda mrefu.
Akikabidhi tuzo hizo za umahili kwa uongozi wa TPA, Dkt. Biteko, ameipongeza Menejimenti na Wafanyakazi kwa ushindi huo na kuitaka TPA kuendeleza juhudi zilizofanya ishinde tuzo hizo kwa mara tatu mfululizo.
Dkt. Biteko amesema ni jambo la fahari kubwa kuona taasisi ya kitaifa ya kiuchumi na kimkakati ikipata mafaniko haya na kueleza furaha yake kwa utendaji wa TPA ambao umetambuliwa na ATE pasipo upendeleo wowote.
Tuzo hizi hutolewa kila mwaka na ATE kwa waajiri kutoka Sekta za Umma na binafsi ambao wameonesha utendaji bora na ubunifu katika mwaka husika.
Ushindi wa TPA ni uthibitisho wa dhamira yake ya kuboresha ustawi wa wafanyakazi, kuboresha mazingira ya kazi, na kuendelea kuchangia maendeleo ya Sekta ya Bandari nchini.
Kwa mara nyingine, TPA imeonyesha kuwa ni mwajiri wa mfano, si tu katika sekta ya umma bali pia kwa jumla katika sekta zote nchini. Pia katika nyakati tofauti, ndani ya mwaka huu, TPA imeshinda tuzo ya mshindi wa tatu kwa taasisi za umma kwa utoaji huduma bora.
Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa mkutano wa siku tatu wa Kikao Kazi kwa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Umma, iliyofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) jijini hivi karibuni.
TPA ni miongoni mwa mashirika yaliyoshiriki katika mkutano huo ambapo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan aliikabidhi Tuzo hiyo kwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPA, Dkt Elinami Minja ambaye aliongozana na Mkurugenzi Mkuu, Bw. Plasduce Mbossa.
Siri nyuma ya tuzo hizi ni uwekezaji katika kuboresha mazingira bora ya wafanyakazi ndani ya Mamlaka hiyo ambapo wafanyakazi wake, mbali na kupata stahiki zao kwa wakati, wamekuwa wakifaidi mambo mbalimbali, ikiwamo huduma bora za Bima ya Afya, motisha, upandishaji vyeo, mafunzo kwa wafanyakazi, likizo, ushirikishwaji katika maamuzi yanayowahusu na michezo.

Na Mwandishi Wetu
Ushirikiano kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Bandari ya Antwerp ya nchini Ubelgiji umepangwa kuimarishwa zaidi ili kuongeza tija na kufungua fursa zaidi za uwekezaji Bandarini.
Hayo yamebainika hivi karibuni mara baada ya ujumbe wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Ubelgiji na Wawekezaji wa Bandari ya Antwerp kufanya ziara katika Bandari ya Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa ziara ya ujumbe, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mbossa amesema ziara ya ujumbe huo umelenga kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya TPA na Bandari ya Antwerp.
Bw. Mbossa pia ametumia fursa hiyo kuelezea fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika Bandari zinazosimamiwa na kuongozwa na Mamlaka.
Maeneo mengine yatakayoguswa na ushirikiano huo, ni pamoja na maboresho ya huduma za Kibandari kulingana na Mkataba wa ushirikiano wa Bandari hiyo ya Antwerp na TPA.
Ushirikiano huo pia umelenga kujikita katika kutoa ushauri elekezi wa namna bora zaidi ya kuyafikia mabadiliko chanya ya huduma za Kibandari hapa nchini, pamoja na ushirikiano wa karibu na Jumuiya hiyo.
Aidha mazungumzo yao yamegusia nia njema ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Maboresho ya Bandari Nchini ambapo Bw. Mbossa ameulezea Ujumbe huo kuhusu fursa zilizopo za Uwekezaji katika Bandari za TPA.
Ujumbe wa Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Ubelgiji, Wawekezaji na Wafanyakazi wa Bandari ya Antwerp uliofanya ziara bandarini, uliongozwa na Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania, Mhe. Peter Huyghebaert na Balozi wa Tanzania katika Ufalme wa Ubelgiji na Jumuiya ya Ulaya, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga ulifanya ziara katika Bandari ya Dar es Salaam kwaajili ya kujionea fursa mbalimbali za uwekezaji katika Bandari hiyo.

Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeshiriki katika zoezi la uokoaji wa wathirika wa ajali ya Ghorofa liliroporomoka katika kata ya Kariakoo, Wilaya ya Ilala, Jijini Dar es Salaam kwa kutoa msaada wa vifaa mbalimbali vya uokoaji.
TPA imetoa msaada wa vifaa vya uokoaji kama kofia ngumu, vizibao, glovu, na mtambo maalum wa kunyanyua vitu vizito ili kusaidia kazi za uokoaji zinazoendelea katika ajali hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, wakati wa kukabidhi vifaa mbalimbali vya uokoaji katika eneo la tukio, Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Abed Gallus, alisema TPA imesikitishwa sana na tukio hilo lililosababisha vifo na majeruhi, na kuwaombea waliopatwa na mkasa huo wapate uponyaji wa haraka.
“TPA, kama wadau wakubwa wa biashara na wafanyabiashara wa Kariakoo na Tanzania kwa ujumla, tumeguswa sana na tukio hili kwa sababu waathirika ni wadau wetu na Watanzania wenzetu,” alisema Bw. Gallus.