TPA YA SAINI MAKUBALIANO YA TARATIBU ZA UENDESHAJI WA KAWAIDA (SOP's) KWA AJILI YA UHAMISHAJI WA SHEHENA HADI KWALA

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetia saini makubaliano ya taratibu za uendeshaji wa Kawaida (SOPs) zilizotayarishwa kwa ajili ya uhamishaji, uhifadhi na usafirishaji wa shehena kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Bandari Kavu ya Kwala, iliyopo Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani.
Hafla hiyo ya utiaji saini makubaliano hayo imefanyika Julai 28,2025 Makao Makuu ya TPA jijini Dar es Salaam, ikihusisha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Shirika la Reli Tanzania (TRC) na waendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, Kampuni za DP World na Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited (TEAGTL).
Akizungumza mara baada ya kusainiwa makubaliano hayo yanayoenda kuifungua Bandari ya Dar esSalaam, Mkurugenzi Mkuu wa TPA Bw.Plasduce Mbossa, amesema taratibu hizi zimetayarishwa kwa pamoja na kila Taasisi imeonyeshwa nini inachotakiwa kufanya katika mchakato mzima wa Uchukuzi wa shehena kutoka bandari ya Dar es Salaam.
Aidha Bw.Mbossa amesema makubaliano hayo yatapunguza muda wa uondoshaji mzigo bandarini, msongamano wa magari makubwa, kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uhudumiaji wa shehena.
Naye Mkuu wa Idara ya Utekelezaji wa TEAGTL Bw.Laksiri Noni amepongeza uamuzi wa kushirikisha wadau wote wanaohusika katika mnyororo mzima wa Uchukuzi wa shehena katika makubaliano hayo.