MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM ATEMBELEA BANDA LA BANDARI YA TANGA MAONESHO YA NANE NANE MOROGORO

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila ametoa pongezi kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw. Plasduce Mbossa na Meneja wa Bandari ya Tanga Bw. Masoud Mrisha kwa utendaji kazi wao uliotukuka hali iliyopelekea kuongezeka kwa ufanisi katika Bandari ya Tanga.
Mhe. Chalamila alitoa pongezi hizo wakati alipotembelea banda la Bandari ya Tanga kwenye Maonesho ya NaneNane Kanda ya Mashariki 2025, yanayofanyika katika Uwanja wa Mwalimu JK Nyerere Mkoani Morogoro.
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya utendaji kazi wa bandari hiyo Mhe. Chalamila alisema kuwa, kuongezeka kwa ufanisi katika Bandari ya Tanga ni pamoja na usimamizi mzuri wa Mkurugenzi Mkuu wa (TPA) pamoja na Meneja wa Bandari hiyo.
Mhe. Chalamila aliongeza kuwa, kuongezeka kwa ufanisi katika bandari hiyo umerahisisha usafirishaji wa shehena ya mazao ya kilimo kutoka Mikoa ya Kanda ya Kaskazini na nchi jirani jambo ambalo ni sifa kwa nchi yetu”.
Aidha Mhe. Chalamila alitoa rai kwa wafanyabiashara nchini kuitumia bandari hiyo kusafirisha mizigo yako kwani usafirishaji kwa njia ya maji hauna mzunguko mrefu na ni salama pia.
Kwa upande wake Afisa Masoko wa Bandari ya Tanga Bw. Ridhiwani Mwasanyagi alimhakikishia Mkuu wa Mkoa huyo bandari ya tanga itaendelea kufanyakazi kwa ufanisi ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwezesha biashara kufanyika kwa ufanisi.
Bandari ya Tanga imekuwa ikisafirisha shehena mbalimbali za mazao ya kilimo kwa uchache kama Mkonge Chai , Kahawa, Macademia hivyo ushiriki wa Bandari ya Tanga kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki 2025, ni kutoa elimu kwa umma na wafanyabiashara wa mazo ya kilimo.