TPA YAPONGEZWA KWA TUZO YA BANDARI SHINDANI BARANI AFRIKA, TALTA YAZINDULIWA RASMI

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imepokea tuzo maalum ya pongezi kwa mchango wake mkubwa katika kuzifanya Bandari za Tanzania kuwa miongoni mwa bandari shindani zaidi katika Ukanda wa mashariki na kusini mwa Bara la Afrika.
Tuzo hiyo imetolewa tarehe 9 Aprili,2025 jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa Chama cha Wataalam wa Lojistiki na Usafirishaji Tanzania (TALTA), hafla iliyohudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya uchukuzi kutoka ndani na nje ya nchi.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, amesema uzinduzi wa TALTA ni hatua muhimu katika kuimarisha weledi, uwajibikaji na utoaji wa huduma bora katika sekta ya uchukuzi nchini.
Ameeleza kuwa serikali inaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa kwenye miundombinu ya uchukuzi ikiwemo reli, barabara, bandari, viwanja vya ndege na vyuo vya mafunzo, hivyo kunahitajika wataalamu waliobobea kushirikiana na serikali katika maendeleo hayo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Usafiri kutoka Wizara ya Uchukuzi, Bw. Andrew Magombana, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, ameahidi ushirikiano wa karibu kati ya wizara na TALTA katika kutekeleza sera, mikakati na maboresho ya sekta hiyo muhimu.
Rais wa TALTA, Bw. Alphonce Mwingira, amesema dhamira ya chama ni kuwaunganisha wataalam wa fani ya lojistiki na usafirishaji kutoka ngazi zote za elimu na kushirikiana kwa karibu na Serikali pamoja na sekta binafsi katika kukuza taaluma hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TALTA, Dkt. Bartholomeo Lufunji, amesisitiza kuwa chama kitaendeshwa kwa kuzingatia maadili, sheria na kufanya tafiti kama nguzo kuu ya ufanisi wa sekta ya uchukuzi.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na wawakilishi kutoka Taasisi za Serikali, sekta binafsi, vyama vya usafirishaji, madereva, wamiliki wa magari ya abiria, na wanafunzi wa vyuo mbalimbali, tuzo mbalimbali zimetolewa kwa Viongozi wakuu wa kitaifa, Wizara, Taasisi za Umma na binafsi kwa kutambua mchango wao katika maendeleo ya sekta ya lojistiki na usafirishaji nchini.