Select your language

Serikali ya Jamhuri ya Msumbiji imeeleza nia yake ya kuendeleza na kukuza ushirikiano uliopo baina yake na Tanzania haswa katika sekta ya Uchukuzi kupitia Ushoroba wa Kusini.

Hayo yamejiri katika Mkutano baina ya Waziri wa Uchumi na Uchukuzi wa Msumbiji Mhe. Basilio Muhate na Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) uliofanyika Mei 06,2025 Makao Makuu ya TPA jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika Mkutano huo Mhe.Muhate amesema ushirikiano katika sekta ya Uchukuzi baina ya nchi hizi utaunganisha Bandari za Mtwara na Nacala hali itakayosaidia ukuaji wa Uchumi wa nchi zote mbili.

Waziri huyo amesema nchi yake ina miundombinu ya kutosha inayoweza kutumika ipasavyo katika shughuli za Uchukuzi wa shehena kupitia Ushoroba wa Kusini.

Awali wakati akitoa salamu za ukaribisho kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Naibu Mkurugenzi Mkuu Dkt.Baraka Mdima, amesema shehena katika Bandari za Tanzania zinasafirishwa kwa njia ya Barabara na reli za TAZARA na Shirika la Reli la Tanzania (TRC) na mchakato wa ujenzi wa gati la kuhudumia meli za kitalii katika Bandari ya Dar es Salaam, upo katika hatua za mwisho.