MHE. RAIS DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZINDUA BANDARI KAVU YA KWALA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Julai 31,2025, ameweka jiwe la msingi la uzinduzi wa Bandari Kavu ya Kwala iliyopo Vigwaza, Kibaha Mkoa wa Pwani.
Bandari hiyo ya kitaifa na kikanda imejengwa katika eneo lenye ukubwa wa hekta 502 ambapo kati ya hizo hekta 120 zimesafishwa na hekta tano zimejengwa kwa kiwango cha zege zikiwa ndani ya eneo la hekta 60 zilizozungushiwa uzio wenye urefu wa kilometa 2.96.
Bandari kavu ya Kwala inatarajiwa kuhudumia na kuhifadhi shehena ya makasha 3500 kwa siku na idadi ya makasha zaidi ya 300,000 kwa mwaka ikiwa ni takribani Asilimia 30 ya Makasha yote yanayopita katika Bandari ya Dar es Salaam.
Bandari hiyo itahudumia pia nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( DRC), Zambia, Malawi, Burundi, Rwanda na Uganda, ambapo nchi zote hizo zimepatiwa maeneo ndani ya Bandari Kavu hiyo ya Kwala.