Chuo cha Bandari kitaanza rasmi kudahili Wanafunzi wapya kupitia mfumo wake mpya wa kidijitali ujulikanao kama “Student’s Information Management System (SIMS)”.

 

Mfumo huo wa kidijitali umezinduliwa hivi karibuni na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaac Kamwelwe (MB) ambae amesema utakiwezesha Chuo kudahili wanafunzi wanaopenda kujiunga na Chuo kutumia njia ya mtandao.

 

Mfumo huo ambao umebuniwa na kutengenezwa na wafanyakazi wa TPA kitengo cha TEHAMA, pia utatumika kukokotoa matokeo ya mitihani na kuanda taarifa ya mwisho wa mwaka wa mafunzo yaani ‘final year transcript’.

 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tovuti ya mfumo huo mpya, Waziri Kamwelwe alisema uwepo wa mfumo huo utasaidia kudhibiti udanganyifu uliokuwa ukifanywa na baadhi ya watendaji wa Chuo wasiokuwa waaminifu.

 

Mhandisi Kamwelwe ameongeza kwamba awali wakati udahili ulipokuwa ukifanywa kwa kujaza fomu kwa mkono ‘manual’, kulikuwa na tatizo la uchakachuaji wa vyeti na upotevu wa pesa.

 

“Wakati wa kufanya maombi ya kujiunga na Chuo kwa kujaza nyaraka “application manual” kuna fomu za maombi zilikuwa zinapotea na kulikuwa na upotevu wa pesa pamoja na tatizo la kuchapisha vyeti feki na baadhi ya Wanafunzi kutohudhuria mafunzo ipasavyo,” amesema Waziri Kamwelwe.

 

Ameongeza kwamba katika kipindi hicho baadhi ya Wanafunzi waliishia kusajiliwa tu na baada ya miaka miwili unamkuta na cheti mtaani lakini sasa kwa kuwepo kwa mfumo huu ni matarajio yetu mambo hayo yatakwisha kabisa.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Bodi ya Magavana ya Chuo na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko amemshukuru Waziri kwa kutenga muda wake na kuzindulia tovuti hiyo ambayo ni nyenzo muhimu kwa chuo katika kuongeza ufanisi na kuondoa mianya ya utendaji mbovu.

 

Mhandisi Kakoko amesema kwamba pamoja na ukweli kwamba Waziri ana mambo mengi lakini bado ameweza kutenga muda na kuthamini jitihada ambazo Mamlaka imezichukua katika kuimarisha utendaji wa Chuo cha Bandari husuani kuzindua mfumo huo muhimu kwa maslahi ya Chuo na Taifa kwa jumla.

 

“Uwepo wa mfumo huu, utarahisisha utendaji kazi wetu kama Chuo na kudhibiti wale wote waliokuwa wakitumia mianya ya kutokuwepo kwa mifumo hiyo, kufanya udanganyifu,” amesema Mhandisi Kakoko.

 

Akizungumzia faida za mfumo huo, mmoja wa wafanyakazi wa TPA ambaye ameshiriki kubuni mfumo huo, Bw. Rainer Mwashu amesema utarahisisha zoezi la udahili wanafunzi na kupata taarifa zao kwa urahisi wakati wowote zikihitajika.

 

“Kupitia mfumo huu, Mwanafunzi ataweza kujisajili kwa ajili ya mwaka wa masomo popote pale alipo…amesema na kuongeza kwamba,…kwa sasa taarifa zote za wanafunzi wa Chuo hiki zitapatikana kidijitali kupitia mfumo huu.”

 

Mbali ya hayo, mfumo huu pia utatumika kuzalisha taarifa ya mwisho ya matokeo ‘final year transcript’, na utawezesha kuoana kwa mifumo ya ndani na nje ya taasisi kama vile NACTE, NECTA na GePG.

Pic 4

Pic 1

Pic 2

Pic 3