Maelezo ya Jumla

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ilianzishwa kwa Sheria ya Bandari Na.17 ya 2004 kusimamia shughuli zote za kibandari nchini. Mamlaka hii inaendesha bandari zinazohudumia Tanzania na nchi zisizo na bandari ikiwemo Zambia, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, Rwanda, Malawi, Uganda na Zimbabwe.

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inatekeleza jukumu la kuhamasisha matumizi ya bandari, kuziendeleza na kuzisimamia ikiwamo, kuingia mikataba ya kisheria ya kukasimu mamlaka yake kupitia utoaji ruksa za uendeshaji wa huduma za bandari kwa kufuata kanuni na mamlaka iliyonayo kwa mujibu wa sheria.  

TPA inasimamia na kuendesha mifumo ya kibandari katika bandari zilizo mwambao wa Bahari ya Hindi na kwenye maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa. Dar es Salaam, Tanga na Mtwara ndio bandari kubwa huku bandari ndogo zikiwa Kilwa, Lindi, Mafia, Pangani na Bagamoyo katika mwambao wa Bahari ya Hindi.

Kazi za Mamlaka

  • Kuanzisha na kusimamia mifumo ya bandari.
  • Kutengeneza miundombinu ya bandari na kutoa huduma.
  • Kujenga bandari mpya na kuziendesha baada ya kuruhusiwa na Waziri.
  • Kujenga, kuendesha na kuhudumia minara, maboya na visaidizi vingine vya kuongozea meli kuingia na kutoka bandarini
  • Kuendesha shughuli za kupakia na kupakua shehena
  • Kutunza shehena mbalimbali za wateja wakati zikiwa katika mikono ya bandari
  • Kushuhudumia shehena kwa niaba ya watu wengine mahali popote kuwe ndani au nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
  • Kwa ruhusa ya waziri mwenye mamlaka TPA watasafirisha shehena ya mizigo au abiria
  • Kutoa vifaa muhimu kwa watu wanaotumia huduma za bandari.

 


Dira Yetu

Kuongoza katika utoaji huduma bora za biashara ya bandari kikanda.

Dhamira Yetu

Kuendeleza na kuendesha bandari zinazotoa huduma za kiwango cha juu na kukuza huduma bora kabisa za usafirishaji katika eneo la Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika.

Kanuni za Maadili

Ili kuwa na ushindani, Mamlaka inaongozwa na kanuni za maadili zinazozingatia uadilifu, weledi, utendaji kazi wa pamoja, uzingatiaji wa wadau, uwajibikaji na uwazi.