Bandari ya Dar es salaam

Hii ni bandari kuu nchini Tanzania yenye uwezo wa kuhudumia tani za metriki milioni 14 za shehena kavu na tani milioni 6.0 za vimiminika,Bandari ina eneo la gati 11 zenye kina kirefu hadi meta 14.5 na jumla ya urefu wa meta 2,600.

Bandari ya Dar es salaam ni lango la kuu la kibiashara, asilimia 95 ya biashara ya kimataifa ya Tanzania inahudumiwa na Bandari hii. Aidha bandari hii inahudumia nchi jirani zisizo na bandari kama vile Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, Rwanda, Malawi, Uganda na Zimbabwe.

Bandari ya Dar es salaam ni kiungo kikuu cha kibiashara si tu kutoka na kwenda nchi za Afrika Mashariki na kati, bali pia na nchi za Mashariki ya kati, Mashariki ya mbali, Ulaya, Australia na Marekani.

Miundombinu ya Bandari 

Nyenzo zilizopo ambazo husaidia uendeshaji wa shughuli za Bandari ya Dar es salaam ni kama ifuatavyo: -
 • Kuna magati ya shehena mchanganyiko (0-5) kwa ajili ya shehena kavu na magari.
 • Magati ya makasha (5-11) .
 • Vihenge vya kuhifadhia nafaka (silos) vyenye uwezo wa tani 30,000, vituo vya makasha vya nchi kavu (ICD) vyenye uwezo wa kuhifadhi 24,300 TEUs na CFs yenye uwezo wa kutunza magari 6,000 kwa wakati.
 • Pia kuna Single Point Mooring (SPM) yenye uwezo wa kuhudumia meli zinazobeba hadi tani 150,000 za mafuta ghafi na mafuta yaliyosafishwa.
 • Bomba la Mafuta Kurasini (KOJ) kwa ajili ya bidhaa ambazo zimesafishwa inapokea meli zenye ukubwa wa tani 45,000 (MT) kwa KOJ1 na tani 5,000 kwa KOJ2.

Kwa jumla uwezo halisi wa Bandari ya Dar es salaam ni kuhudumia zaidi ya tani milioni 18 za shehena kama ifuatavyo: -

 • Shehena za kawaida tani milioni 5.2
 • Makasha tani milioni 6.8
 • Vimiminika tani milioni 6.0

Mgawanyiko wa Miundombinu ya Bandari

Kuna eneo la gati lenye urefu wa mita 2,600 na limegawanywa kama ifuatavyo:
  

Kitengo cha Shehena Mchanganyiko

Sehemu hii ya bandari ina gati la urefu wa mita 797 lenye mgawanyiko wa magati makuu manne (4), maghala ya kuhifadhia shehena zinazopitia kwenda nchi nyingine yenye ukubwa wa meta za mraba 64,463.5 na hifadhi ya wazi yenye ukubwa wa meta za mraba 201,613

Kitengo cha Makasha

Bandari ya Dar es Salaam, kuna Vituo viwili (2) vya Makasha vinavyoendeshwa na TPA Yaani; Kitengo cha Makasha I (Gati Nambari 5 hadi 7) na Kituo cha Pili cha Makasha (Gati Nambari 8 hadi 11). Terminal II ya Kontena ina urefu wa mita 725 na uwezo na uwezo wa kushughulikia zaidi ya TEU 660,000 kwa mwaka kulingana na, miongoni mwa mengine, aina ya vifaa vilivyotumwa, Mifumo ya Tehama.

 

Kitengo cha Nafaka

Bandari ya Dar es Salaam ina miundombinu ya kisasa ya kushughulikia shehena ya nafaka kiautomatiki. Mifumo iliyopo pamoja na vihenge inapokea tani 30,000 za nafaka. Nafaka inaweza kupakuliwa na kujazwa kwenye magunia kwenye eneo la gatini kwa wastani wa zaidi ya tani 2,000 kwa saa 24 au kuhamishwa kwa kutumia malori. Vihenge vipo katika hali inayotakiwa kimataifa ya uhifadhi nafaka.

 

Kitengo cha Mafuta

Kuna maeneo mawili yanayotumika kupakua shehena ya mafuta. Kuna Single Point Mooring (SPM) na Kurasini Oil Jetty (KOJ). Katika eneo la SPM meli ya mafuta hushusha karibu na ufukwe. SPM ina uwezo wa kupokea meli za mafuta zenye uzito hadi tani za metriki 150,000 (MT) na kasi ya kupakua ya kiwango cha mita za ujazo 2,500 kwa saa kwa mafuta ghafi.

SPM imeunganishwa na viwanda vya kusafishia mafuta vya Dar es Salaam na Ndola - Zambia, Eneo jingine ni la Kurasini, KOJ ambalo uhudumia shehena za mafuta yaliyosafishwa ina uwezo wa kusukuma tani 750 kwa saa. Linaweza kushughulikia meli za mafuta hadi zenye tani 45,000 (MT).

 

Maeneo ya Kuhifadhia

Bandari inatoa hifadhi za wazi na zilizofunikwa. Ina vihenge kwa ajili ya nafaka na eneo la kuhifadhia makasha, magari na shehena mchanganyiko.

  

Vyombo vya Kuhudumia na Kuelekezea Meli

Bandari ya Dar es Salaam inahudumuiwa na boti maalum za kuvutia meli (Tugs), boti za nahodha na boti za ulinzi/doria. Pia kuna miundombinu ya kuelekezea meli bandarini (Navigation Aids). Miundombinu hiyo ni pamoja na maboya, milingoti ya kuongozea meli, alama za ishara na minara ya taa.

  

Vyombo vya Kushughulikia Shehena za Kawaida

Vyombo vikuu vya kuhudumia shehena za kawaida ni winchi kubwa, foko, trekta, matela, grabs, hoppers, Bagging units, malori,mizani, na mikanda ya kuhamishia mizigo.

  

Vyombo vya Kushughulikia Makasha

Bandari ina vifaa vya kuhudumia makasha kama vile winchi kubwa (Ship to shore gantry cranes -SSGs), winchi kubwa za matairi (Rubber tyred gantry cranes RTGs) na winchi kubwa inayotembea katika reli (Rail Mounted Gantry Crane RMG), Gottwalds, malori ya usafirishaji malori yenye foko, matela yanayotumika barabara kuu, matrekta na matela.

  

Miradi Mikuu ya Bandari

 • Uboreshaji wa Bandari ya Dar es salaam

  Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inatekeleza miradi mbalimbali mikuu kama ilivyoelezwa kwenye utafiti wa mpango mkuu wa Bandari wa Taifa (PMP) uliofanywa na Royal Haskoning, Februari, 2009 na kufanyiwa Maboresho mwaka 2020.

   

  Utafiti huo umeweka mkakati wa muda urefu wa bandari za Tanzania kuwa na uwezo wa kukidhi matarajio ya mahitaji. Miongoni mwa miradi hiyo ni Mradi wa Lango la Bahari la Bandari ya Dar es Salaam (DMGP) DMGP utaboresha matumizi na ufanisi kwa kuibadilisha bandari kuwa ya kiwango cha kimataifa yenye ufanisi mkubwa.

   

  Baadhi ya miradi itakayofanya bandari kuwa ya kisasa ni pamoja na kuimarisha na kuongeza kina cha magati ya 1 – 7 na gati la RoRo, uzoaji taka na tope kwenye njia ya kuingilia meli, mzunguko wa kugeuza meli, kuimarisha na kuongeza kina cha magati namba 8 – 11 na kujenga gati jipya la kuhudumia mafuta.

 • Uboreshaji wa Uendeshaji wa kisasa wa huduma za shehena kavu

  Ndani ya mradi huo TPA itaendesha kisasa shughuli za huduma za shehena kavu kwa kutumia teknolojia ya kisasa yenye ubunifu wa hali ya juu ya usafirishaji.

 • Ujenzi wa Chelezo

  Hii ni miundombinu kwa ajili ya ukarabati na matengenezo ya vyombo vya kuhudumia meli na hivyo kuongeza ufanisi wa utendaji wa Bandari.

 

Kwa maelezo zaidi wasiliana na:

Mkurugenzi wa Bandari -Dar es Salaam,
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),
S.L.P 1130 Dar es Salaam,
Dar es Salaam, Tanzania.

Simu: +255 22 2113642
Faski: +255 22 2113646
Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.