Kurudisha Fadhila kwa Jamii

Taarifa Kwa Kina

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kama zilivyo taasisi zingine za kibiashara, inajishughulisha na shughuli za kijamii, kwa kurudisha fadhila kwa jamii (CSR)inayoizunguka.

Utaratibu wa TPA wa kurudisha fadhila kwa jamii unaangalia miradi isiyo ya kibiashara yenye uhalisia wa kimaendeleo, ili kuinua maisha ya jamii. Miradi hii hutumia rasilimali za shirika ili kunufaisha jamii nzima.

Ili kusaidia jitihada za serikali za kuleta maendeleo, TPA inaelekeza misaada yake katika maeneo makuu manne ya afya, elimu, ustawi wa jamii na maafa. TPA ili kutekeleza hayo yote inaongozwa na maadili ya kazi yanayosisitiza utawala bora, uadilifu, uaminifu, kuaminika, kumjali mteja na kufanya kazi kwa pamoja. Kutokana na hali hiyo TPA hujikita katika kujipambanua kama taasisi imara inayojali wateja wake na kuwahudumia kwa kufuata utaratibu na misingi iliyojiwekea.

Kwa hiyo kila shughuli ya urudishaji fadhila kwa jamii (CSR) ni lazima iwe na madhumuni. Kutokana na mazingira hayo shughuli hiyo ni lazima ipangwe kwa ajili ya utekelezaji timilifu, lazima ipimike. Shughuli yoyote ya CSR lazima ipangwe na kutekelezwa kwa namna ambayo inaleta manufaa kwa pande zote mbili na kuanzisha uhusiano endelevu wenye manufaa kijamii na kitaifa. Ndio kusema Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) itashiriki tu katika miradi itakayoimarisha uwezo wa jamii kuchangia maendeleo yao, kijamii na kiuchumi.

TPA kwa kufanya shughuli za urejeshaji wa fadhila itahakikisha kunakuwapo na matokeo chanya katika miradi itakayosaidia jamii inayoizunguka kuhakikisha kuna mahusiano mazuri na jamii hiyo.

Kwa kuwa mipango ya urudishaji fadhila kwa jamii wa TPA inahusisha miradi isiyo ya kibiashara, mradi husika unatakiwa kuwa chachu ya kuleta maendeleo na hauna sura ya kibiashara.