dg

Ujumbe Kutoka Kwa Mkurugenzi Mkuu

 

Mpendwa Mteja, Karibu Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeanzishwa chini ya Sheria ya Bandari namba 17 ya mwaka 2004. Sheria hii ilitoa mamlaka kwa TPA kuanzisha na kuendesha mifumo na huduma za bandari zinazohudumia Tanzania bara na nchi zisizo na bandari za Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, Rwanda, Malawi na Uganda. Nchi nyingine zinazotumia Bandari za Tanzania ni Zimbabwe, Sudan Kusini na Comoro.

TPA inasimamia utoaji huduma za bandari nchini Tanzania kuanzia baharini na kwenye maziwa na katika uendeshaji huo Dar es salaam ndio bandari kuu na kitovu cha bandari zote.

Bandari nyingine kubwa kwenye mwambao wa bahari ni Tanga na Mtwara wakati bandari ndogo za kwenye bahari ni Kilwa, Lindi, Mafia, Nyamisati, Kisiju, Bagamoyo, na Pangani.

Bandari za Ziwa Viktoria ni pamoja na Bandari za Mwanza Kaskazini na Kusini, Nansio, Kemondo Bay, Bukoba na Musoma kwenye Ziwa Victoria; huku Kigoma, Kibirizi, Kabwe, Kipili, Kagunga, Karema na Kasanga zikiwa kwenye Ziwa Tanganyika na Bandari ya Itungi, Kiwira, Manda Liuli na Mbamba Bay zikiwa kwenye Ziwa Nyasa.

Hivi sasa, Mamlaka inatekeleza majkumu yake kwa namna mbili, kwanza kama mwendeshaji na pia mkodishaji lengo likiwa ni kukuza usimamizi na uendeshaji madhubuti wa bandari ziliozopo baharini,nchi kavu na ziwani.

Aidha inawajibika kutoa huduma zinazohusiana na upakiaji na upakuaji wa mizigo na abiria, kuendeleza, kukuza, na kusimamia miundombinu ya bandari na menejimenti bora, kudumisha ulinzi na usalama wa bandari.

Bandari ya Dar es Salaam ni lango kuu la Biashara ya Kimataifa kwa Afrika Mashariki (kwa kuagiza na kuuza nje). Kwa sasa TPA inaendesha na kusimamia Bandari zote (Bahari na Ziwa) katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Bara) na inabaki kuwa mdau mkuu wa viwanda katika sekta ya usafiri Kanda ya Afrika Mashariki.

Ni wajibu wetu kutoa huduma zilizotukuka wateja wetu na kuhakikisha kuna usalama na ufanisi kwa kutoa huduma za hali ya juu zinazoambatana na kasi kwa kuwa na teknolojia ya kisasa, vifaa vya kisasa zaidi vya bandari, miundombinu ya bandari na mifumo rafiki ya Tehama ambayo inachangia kuwa na muda mfupi wa kuhudumia shehena.

TPA kwa sasa inaendesha miradi mikubwa ya upanuzi na maendeleo ya bandari zote za bahari na maziwa. Uboreshaji na uendelezaji wa Bandari ya Dar es Salaam kupitia Mradi wa Lango la Bahari la Dar es Salaam (DMGP) utatuwezesha kuongeza kina cha maji hadi mita 14.5, kupanua njia ya kuingilia, kuimarisha gati 1-11 na ujenzi wa gati mpya ya magari maalumu (Ro-Ro), uboreshaji wa bandari ya Tanga kwa kuongeza kina na kuimarisha gati. Uwekezaji huu utaongeza zaidi uwezo wa Bandari kushughulikia meli na mizigo zaidi.

TPA imedhamiria kusonga mbele, ikijikita katika kuchangia sera ya ukuaji wa Viwanda inayoongozwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan. Mipango yetu ya muda mrefu ni kuona ukuaji wa biashara ya makasha, shehena ya jumla, na biashara ya mafuta na gesi na kujikita katika bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima hadi hongolea Tanga.

Pamoja na majukumu yetu, na kasi ya kutekeleza hatujawahi kutetereka katika utoaji wa huduma bora kwa wateja wetu. Kiwango cha huduma zetu kwa wateja kinaweza kuonwa katika mkataba wetu wa huduma.Aidha tutaendelea kupitia ubora wa kazi zetu na kupimwa kupitia a Huduma kwa Wateja. Pia tutazingatia kwa makini katika kuelewa mahitaji ya wadau na wateja wetu ili kuendelea kuwahudumia vyema.


- Bw. Plasduce M. Mbossa