Baraza kuu la Majadiliano (CJIC) la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) limefanya kikao cha kawaida cha Hamsini na Saba (57) kinachofanyika mjini Morogoro.
Kikao hiko kimelenga kupitia na kuthibitisha Utekelezaji wa Makubaliano ya Kikao cha kawaida cha Hamsini na sita (56) kilichofanyika Disemba 2024.
Pamoja na mambo mengine, Baraza hilo limewaaga wajumbe wake ambao ni Afisa Mwandamizi Bandari ya Kyela Bw. Florian Mloka na Katibu wa DOWUTA Tawi la Dar es Salaam Bw. Hassan Ahmed kwa kuhitimisha muda wa wao wa utumishi kisheria katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).




Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kushirikiana na waendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, DP World na Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited (TEAGTL), wameendesha kampeni ya kimasoko katika mji wa Lubumbashi, DR Congo.
Ziara hiyo ililenga kusikiliza changamoto za wateja na wadau wa biashara, pamoja na kuwasilisha maboresho makubwa yaliyofanywa katika Bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na Kigoma.
Akifungua mkutano huo, Konseli Mkuu wa Tanzania mjini Lubumbashi, Bw. Magubilo Muroba, alipongeza ushirikiano kati ya bandari za Tanzania na wafanyabiashara wa DR Congo, uliosababisha ongezeko la mizigo kwa asilimia 43 kutoka tani milioni 4.1 mwaka 2023/24 hadi milioni 5.9 mwaka 2024/25.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Josephat Lukindo, alisisitiza dhamira ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kutoa huduma za kisasa. Ushirikiano wa TPA na waendeshaji wake, ukiungwa mkono na uwekezaji wa mitambo ya kisasa, umefanya muda wa kuhudumia meli za makasha kupungua hadi wastani wa siku tatu.
Mbali na mkutano, ujumbe huo ulitembelea kampuni kubwa za usafirishaji ikiwemo Impala Cargo Terminal na Conexas Terminal, ambazo zote ziliridhishwa na huduma zitolewazo na kuahidi kuendeleza ushirikiano na bandari za Tanzania.


Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inashiriki Kongamano la Kitaifa la Wadau wa Uchumi wa Buluu 2025, linaloenda sambamba na maonesho ya shughuli zinazofanywa na Taasisi shiriki, na linafanyika kwa siku mbili Jijini Dar es Salaam.
Kongamano hilo linaloenda na kauli mbiu ya “Bahari Yetu,Fursa Yetu, Wajibu Wetu: Kuanzia 2021 hadi 2025”, limefunguliwa Septemba 10, 2025 na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Mhawi.
Kwa upande wa Maonesho, Banda la TPA limekuwa kivutio kwa Wadau mbalimbali wa Uchumi wa Buluu kutembelea kwa ajili ya kupata maelezo kuhusu majukumu ya Mamlaka na shughuli mbalimbali za utekelezaji Bandarini.




Balozi wa Urusi hapa nchini Mhe. Andrey Avetisyan, ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kuendelea kuiboresha Bandari ya Mtwara, inayoendelea kutoa huduma bora na za ufanisi.
Balozi Avetisyan, ametoa pongezi hizo, tarehe 8 Septemba, 2025 alipofanya ziara ya kutembelea Bandari ya Mtwara, ambapo ameongozana na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Patrick Kenan Sawala pamoja viongozi mbalimbali wa ngazi ya Mkoa.
Amesema pia ameridhishwa na utendaji kazi wa Bandari ya Mtwara, na kueleza kubaini fursa mbalimbali zilizopo katika Bandari hiyo, ambazo zikitumiwa vizuri zitaleta maendeleo na ongezeko la mapato zaidi.
Kwa upande wake, Meneja wa Bandari ya Mtwara Bw. Ferdinand Nyathi, ameelezea hali ya utendaji kazi wa Bandari hiyo kuwa umeimarika zaidi , kufuatia maboresho mbalimbali yaliyofanywa na Serikali ambayo yameongeza tija na ufanisi katika utoaji wa huduma.




Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) leo tarehe 03 Septemba 2025 limefanya kikao cha Thelathini na nane (38) kilichofanyika mjini Morogoro.
Kikao hiko cha siku mbili kimelenga kujadili na kupokea utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2024/2025 na mpango na bajeti kwa mwaka 2025/2026.
Baraza hilo limeongozwa na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala Bw. Mbarikiwa Y. Masinga kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA Bw.Plasduce M. Mbossa.






EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"