Na Mwandishi Wetu Gavana wa Jimbo la Kivu Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo - DRC Mhe. Théo Ngwabidje Kasi, ametoa Rai kwa Wawekezaji na Wafanyabiashara wa DRC na Tanzania kuzitumia vema fursa zilizopo kati ya nchi hizo kuimarisha na kuongeza uwekezaji na Biashara zao. Gavana Kasi ametoa Rai hiyo tarehe 29 Aprili, 2023 wakati akifungua kongamano la Uwekezaji na Biashara Mjini Bukavu ambapo amesema Wakuu wa nchi hizi mbili wameweka dhamira ya dhati pamoja na mambo mengine kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa kuimarisha Uwekezaji, Biashara na Masoko, hivyo ni vema Wananchi wa nchi zote mbili wakatumia fursa hiyo. " Biashara ni kwa maendeleo ya Nchi zetu na Biashara nyingi inatoka Tanzania kuja Kongo na kutoka huku kwenda Tanzania, hali ya usalama ipo vizuri na hivyo kurahisisha Biashara na usafirishaji Kati ya nchi hizi mbili". Amesema Gavana Kasi. Naye Balozi wa Tanzania Nchini DRC Mhe. Saidi Juma Mshana amesema kufanyika kwa kongamano hilo ni Katika kutekeleza maagizo na maelekezo ya MaRais wa nchi hizi mbili kuhusu Tume ya pamoja ya kudumu ya ushirikiano kwa lengo la kudumisha na kuimarisha uhusiano, ushirikiano na kuboresha miundombinu ikiwemo Bandari , Reli na Barabara ili kurahisisha Biashara na Masoko Kati ya nchi hizi. " Ni muhimu kwa nchi zetu hizi kuendelea kushirikiana na kwa Wafanyabiahara fursa zilizopo zitumike kwa ajili ya manufaa ya nchi zote mbili ikiwemo uwepo wa Bandari ili kurahisisha Biashara na masoko " . Amesema Mhe. Balozi Mshana. Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dkt. Jilly Maleko amesema Kongamano hili litumike kuimarisha mahusiano na Diplomasia ya kiuchumi na hivyo kukuza Biashara Kati ya nchi hizi mbili. "Nimekuja kutoka Burundi kushiriki nanyi Katika kongamano hili kwa sababu ya Shehena kubwa inayokuja Jimbo la Kivu kusini kutoka Tanzania inapitia Katika nchi ya Burundi, sasa changamoto zote zinazowakabili ni wajibu wa Balozi kuzifanyia kazi ili kurahisisha mazingira ya biashara na kukuza biashara hizo " Amesema Mhe. Balozi Dkt. Maleko. Katika kongamano hilo Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania -TPA imeshiriki vema ambapo Wawakilishi wake Katika nchi za DRC na Burundi wamewasilisha mada kuhusu thamani na umuhimu wa kutumia Bandari za Tanzania kusafirisha Shehena kufuatia maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali Katika Bandari Nchini na nafuu kubwa ya tozo za Bandari inayotolewa kwa Wasafirishaji wa Shehena wa DRC. Ushiriki wa TPA Katika kongamano hili ulikusudia kukutana na Wasafirishaji wa Bidhaa kwa njia ya maji wa Jimbo la Kivu Kusini na kupata maoni yao kuhusu huduma za Bandari zitolewazo na TPA. Kongamano hilo la siku moja limeshirikisha Serikali ya Jimbo la Kivu kusini- DRC, Balozi za Tanzania nchini DRC na Burundi, TPA , CRDB Burundi na Chemba ya wenye Viwanda, Biashara na Kilimo- TCCIA Mkoa wa Kagera pamoja na Shirikisho la Wafanyabiashara wa Kongo - FEC. Kongamano hilo limelenga kutafuta masoko ya huduma za Taasisi za Tanzania pamoja na masoko ya bidhaa za viwandani na Mazao ya kilimo ya Tanzania Nchini DRC. Mwisho