Kampuni ya China Harbour Engineering leo imekabidhi kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) mradi mkubwa wa kimkakati wa maboresho ya Bandari ya Tanga baada ya kazi kubwa ya utekelezaji wa mradi huo. Mradi huo ulihusisha uongezaji kina wa mlango wa bandari (entrance channel) kutoka mita 3 mpaka mita 13, sehemu ya kugeuzia meli (turning basin) na uongezaji wa kina cha gati kutoka mita 3 mpaka mita 13. Lengo la mradi huo ni kuhakikisha Bandari ya Tanga inahudumia meli kubwa na gatini na shehena kubwa ya mzigo kutoka tani 750,000 za sasa mpaka tani milioni tatu kwa mwaka. Akipokea mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Juma Kivajara ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa na Kampuni ya CHEC kwa utekelezaji wa mradi huo kwa ufanisi na kiwango bora. Akiongea katika makabidhiano hayo, Eng. Kijavara amewataka wafanyakazi wa Bandari ya Tanga kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza kiasi cha shehena ya mzigo kulingana na malengo yaliyowekwa na Mamlaka. Aidha Eng. Kijavara amesema TPA itaendelea kuboresha Bandari ya Tanga kwa kujenga gati mpya ya urefu wa mita 250, gati ya meli za abiria yenye urefu wa mita 50 pamoja na ujenzi wa "One Stop Center". Mwisho