Mwandishi Wetu Bodi ya Wakurugenzi ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imeeleza kuridhishwa kwake na utendaji kazi wa Bandari ya Dar es Salaam. Akizungumza na mwandishi wa TOVUTI ya TPA, Mwenyekiti wa Bodi hiyo ambaye pia ndiye Gavana wa Benki hiyo Kuu, Bw. Emmanuel Tutuba, amesema kuwa Bodi yake imeridhishwa na utendaji kazi wa Bandari ya Dar es Salaam hususani mchango wake Katika ukuaji wa uchumi wa nchi. Gavana Tutuba amesema kwamba Bodi yake pia imejiridhisha kuwa Bandari za TPA kupitia uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali, zinaweza kuchangia kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa fedha za kigeni nchini kupitia mapato yatokanayo na Bandari. “Mapato mengi yanakusanywa kupitia shughuli za kibandari na hapa tumejionea wenyewe utendaji kazi wa Bandari hii na kazi nzuri inayofanyika hapa kulingana na majukumu yetu ya msingi ambayo ni kusimamia masuala ya uchumi, amesema Gavana Tutuba na kuongeza kwamba, tumejadiliana kwa kina na kuangalia namna ambavyo Bandari inavyoweza kuchangia zaidi kwenye ukuaji wa uchumi hasa kupitia upokeaji wa mizigo kutoka nje na kuiondosha kwa haraka kuipeleka kwenye maeneo husika.” Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPA, Balozi na IGP Mstaafu Ernest Mangu, amesema ziara hiyo imekuwa na tija kwa TPA hasa kupitia ushauri uliotolewa kwa TPA juu ya namna bora zaidi ya kuongeza mapato kupitia Bandari zilizopo hapa nchini na kuchangia zaidi katika ukuaji wa uchumi wa nchi. “Kuna maeneo ambayo Bodi ya BOT wametupa ushauri na tumeuchukua, na tutautekeleza Kwani lengo kuu ni kuboresha utendaji wetu na kuongeza mapato na hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi,” alimesema Balozi Mangu. Katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya BOT, Gavana Tutuba aliongozana na Naibu Gavana, Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha wa BOT Bi. Sauda Kassim Msemo na Wajumbe wa Bodi yake huku kwa Upande wa TPA mbali na Mwenyekiti wa Bodi Balozi Ernest Mangu, alikuwepo pia Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mkeli Mbossa, Mkurugenzi wa Bandari ya DSM, Bw. Mrisho Mrisho pamoja na wajumbe wengine wa Menejimenti ya TPA. Mwisho