Serikali imepanga kuanza ujenzi wa gati 10 mpya katika Bandari ya Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuifanya sekta ya uchukuzi kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa.

Kauli ya Serikali imetolewa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile (Mb), tarehe 11 Disemba 2025, alipomuwakilisha Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, katika hafla ya uzinduzi wa mtambo mpya wa Reach Stacker uliofanyika katika Bandari Kavu ya Zambia Cargo & Logistics Limited, jijini Dar es Salaam.

Amefafanua kuwa ujenzi huo wa gati 10 mpya utaifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa na jumla ya gati 22 zitakazowezesha kuhudumia meli kwa ufanisi na kuongeza uwezo wa upitishaji mizigo.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa matanki 15 ya kuhifadhia na kusambaza mafuta yaliyopo Kigamboni, ujenzi wa Bandari mpya ya Bagamoyo, ujenzi wa gati jipya eneo la Kisiwa Mgao Mkoani Mtwara na bujenzi wa Bandari mpya ya Mbamba Bay.

Aidha, Naibu Waziri Kihenzile ameihakikishia Serikali ya Zambia kuwa Tanzania itaendelea kudumisha ushirikiano wa muda mrefu katika sekta ya uchukuzi na biashara, ushirikiano ambao utanufaisha wananchi wa pande zote mbili za Tanzania na Zambia.