Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezipongeza Taasisi, Mashirika ya Umma ikiwemo Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Kampuni ambazo Serikali inamiliki hisa, kwa utendaji makini na kuonyesha kuridhishwa kwake na mwenendo ambao ni matokeo ya utekelezaji wa maelekezo yake kwa Taasisi na Mashirika ya Umma kuongeza tija na ufanisi katika utendaji. 

Mhe. Rais ametoa pongezi hizo tarehe 10 Juni, 2025, Ikulu Jijini Dar es Salaam, katika hafla ya kupokea Gawio la Asilimia 15 ya Mapato ghafi ya Taasisi na  Mashirika ya Umma kwa mwaka 2025 ambapo TPA imeibuka kinara katika Taasisi zinazotoa gawio la Asilimia 15 ya mapato ghafi kwa kutoa gawio la Shilingi bilioni 181.5 kutoka Shilingi bilioni 153.917 mwaka 2024. 

Huu ni mwaka wa tatu mfululizo kwa TPA kuibuka kinara kwa kutoa gawio kwa Serikali, jambo linalotajwa kuchangiwa na ushirikishwaji wa sekta binafsi ikiwemo DP World na Tanzania East Africa Gateway Terminal katika uendeshaji wa shughuli za Bandari.