Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imeahidi kuendeleza ushirikiano utakaochangia kuimarika na kuukua kwa sekta ya Uchukuzi baina yake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususani bandari na reli kupitia mpango kazi wa FOCAC.

Hayo yamejiri katika kikao baina ya Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa na Naibu Waziri wa Biashara wa China Mhe.Tang Wenhong pamoja na ujumbe wake, makao makuu ya TPA Jijini Dar es Salaam, tarehe 27 Aprili 2025.

Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na China katika sekta ya usafirishaji na biashara hasa kupitia maboresho ya miundombinu ya bandari, Reli ya TAZARA na Ujenzi wa Reli ya kisasa ya SGR.

Katika mkutano huo, viongozi hao walijadili mikakati ya kuharakisha utiaji saini wa Mikataba ya miradi ya maboresho na ukarabati wa Reli ya TAZARA, kuongeza matumizi ya bandari katika kusafirisha shehena, ambapo Naibu Waziri wa Biashara wa China Mhe. Wenhong, amesisitiza dhamira ya serikali yao kuendelea kuwekeza nchini Tanzania, huku akieleza kuwa maendeleo yaliyofanyika kwenye bandari, Ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR unaoendelea, na ukarabati wa reli ya TAZARA utakaofanyika, vitakuwa kichocheo kikubwa cha biashara na mahusiano ya kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania Mhe. Prof. Mbarawa, ameeleza kuwa ushirikiano uliopo baina ya Nchi hizi mbili ni muhimu kwa uchumi wa Taifa na unafungua fursa zaidi kwa wafanyabiashara wa ndani na wa kanda nzima ya Afrika Mashariki.

Mkutano huo umemalizika kwa pande zote mbili kuahidi kuimarisha zaidi urafiki na ushirikiano wa kimaendeleo. Katika Mkutano huo Waziri wa Uchukuzi aliambatana na baadhi ya Viongozi na watumishi kutoka TPA, TAZARA na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.