Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, ametoa wito kwa Wafanyakazi na Wananchi wa Mkoa huo, kulinda miundombinu ya Bandari ya Tanga kwani ni tunu ya Mkoa huo kiuchumi.

Balozi Dkt. Burian ametoa wito huo, wakati wa mapokezi ya baada ya Meli ya MV ELISAR iliyotia nanga bandarini hapo ikiwa na Shehena Tani 33,000 ( Elfu thelathini na tatu) ya mizigo mchanganyiko.“Ujio wa meli hii ni matunda ya uwekezaji uliofanyika katika Bandari ya Tanga, kwahiyo sisi kama watendaji na wananchi kwa jumla tuone ni tunu katika Mkoa wetu hivyo, hatuna budi kutunza miundombinu ya bandari yetu” Alisema Balozi Burian.

Aidha Balozi Burian alisema kuwa Bandari ya Tanga licha ya kuiletea sifa Tanzania pia imekuwa ikinufaisha wananchi wa Tanga mmoja baada ya mwingine kuanzia kwenye ajira mpaka kwenye mzunguko wa pesa kwa wananchi.Pia Balozi Dkt. Burian amewataka wadau mbalimbali kuendelea kuitumia bandari hiyo ambayo inazidi kusogeza huduma zake baada ya hivi karibuni kuzindua reli ya mizigo kutoka bandarini hapo na kuunganisha na reli ya kati kupitia Ruvu kwenda Mikoa ya Magharibi na nchi jirani.

Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Meneja wa Bandari ya Tanga Bw. Salehe Mbega, alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa Bandari ya Tanga imejipanga vyema katika kuihudumia meli hiyo kuanzia wafanyakazi na vitendea kazi vya kisasa.

 Meli hiyo yenye urefu wa mita 187 imeletwa na Kampuni ya Seafront Shipping Services LTD na imetia nanga bandarini hapo ikitokea nchini China ikiwa imebeba mizigo mchanganyiko kama Magari na Mitambo mbalimbali ya viwandani.