Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) IGP Mstaafu Mhe.Balozi Ernest J. Mangu, ameongoza wajumbe wa Bodi hiyo katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa Bandari ya Mtwara, tarehe 9 Oktoba 2025.

 Ziara hiyo ilihusisha kutembelea Bandari hiyo na kupata taarifa za utendaji kazi wake, pamoja na kutembelea Mradi wa Usanifu na Ujenzi wa Bandari ya Kisiwa Mgao ili kushuhudia maendeleo ya utekelezaji wake.

Mhe. Balozi Mangu alieleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa Mradi huo, ambao unatarajiwa kuhudumia tani milioni 2.5 za shehena kwa mwaka utakapokamilika.

 Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Mha. Dkt. Baraka Mdima, ameeleza kuwa TPA itaendelea kuzisimamia na kuziendeleza Bandari zote nchini, ikiwemo Bandari ya Mtwara, ili kuendana na ongezeko la mahitaji ya huduma za bandari na kuiwezesha sekta ya bandari kutoa mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

 Akieleza matarajio yaliyopo, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Bw. Ferdinand Nyathi, amesema kuwa mwelekeo na mtazamo wa kimasoko kwa sasa ni chanya, kwa kuwa Bandari imeanza kuhudumia shehena ya mafuta yanayosafirishwa kwenda nchi jirani za Zambia na Malawi, hatua ambayo inazidi kufungua milango ya Bandari kwa kuhudumia shehena zaidi katika nchi hizo.