Meneja wa Bandari ya Tanga, Bw. Salehe Mbega, amesema kuwa, Bandari ya Tanga itaendelea kuweka mazingira rafiki ya utoaji huduma bora ili kuweza kuvutia wateja wengi zaidi kutumia bandari hiyo.

Bw. Mbega amesema hayo wakati wa kikao cha Kamati ya Maboresho ya Bandari ya Tanga (PIC) kinachojumuisha wadau wa bandari hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano katika Jengo la Bandari (Bandari House).

Amesema kuwa, Bandari ya Tanga itazidi kuboresha huduma zake kwa kuongeza vifaa vya kisasa vya kupakia na kupakua mizigo, kuboresha miundombinu inayotumika kuhifadhi mizigo ya wateja pamoja na kupunguza siku za kuhudumia meli inapokuwa bandarini.

Kwa upande wao wadau wa Bandari ya Tanga wamepongeza juhudi zinazofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania katika kuhakikisha Bandari ya Tanga inatoa huduma bora kwa wateja ikiwemo kuhudumia meli kwa muda mfupi.