WAZIRI MKUU AVUTIWA NA UFANISI SEKTA YA UCHUKUZI
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ( Mb), ameipongeza Wizara ya Uchukuzi na taasisi zake, ikiwemo Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kwa hatua zinazopigwa katika kuendeleza miundombinu na kuboresha huduma za uchukuzi, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi, ufanisi na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi inayochochea ukuaji wa uchumi kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dkt. Nchemba ametoa pongezi hizo Novemba 16, 2026, jijini Mwanza, wakati akifungua Mkutano wa 19 wa Tathmini ya Pamoja ya Sekta ya Uchukuzi (JTSR), ambapo amesisitiza umuhimu wa kuimarisha muunganiko wa bandari, reli, barabara, viwanja vya ndege na usafiri wa majini ili kurahisisha biashara, kupunguza gharama za usafirishaji na kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha usafiri na usafirishaji wa mizigo katika Afrika Mashariki na Kati.
Katika mkutano huo, Waziri Mkuu ameitaka TPA na taasisi nyingine zilizo chini ya Wizara ya Uchukuzi kuhakikisha mipango na uwekezaji vinaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akibainisha kuwa mafanikio ya uwekezaji hayapaswi kupimwa kwa idadi ya miradi inayotekelezwa pekee, bali pia kwa mchango wake katika kuongeza ufanisi wa huduma, kupunguza muda na gharama za usafirishaji na kufungua fursa zaidi za kiuchumi kwa wananchi.
Aidha, Dkt. Nchemba amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji na uendeshaji wa miundombinu ya uchukuzi kupitia mifumo bunifu ya ufadhili na ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP), ili kuongeza uwezo wa utekelezaji wa miradi na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa jumuishi, salama na endelevu.
Awali, Waziri Mkuu alitembelea banda la maonesho la TPA na kupata maelezo kuhusu shughuli za kibandari, maendeleo ya huduma za bandari na matumizi ya mifumo jumuishi katika kurahisisha na kuongeza ufanisi wa utoaji wa shehena bandarini, hatua zinazochangia kuimarisha nafasi ya bandari za Tanzania katika biashara ya kikanda na kimataifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa Mnyaa, amesema Serikali imepiga hatua katika kuboresha miundombinu ya bandari, reli, barabara, anga na usafiri wa majini, akibainisha kuwa uwekezaji huo unalenga kuimarisha muunganiko wa maeneo mbalimbali, kuchochea biashara na kuiweka Tanzania katika nafasi ya kimkakati ya kuwa kitovu cha usafirishaji Afrika Mashariki na Kati.
Mkutano huo unaofanyika Novemba 16–18, 2026, wenye kaulimbiu isemayo “Kuharakisha Utoaji wa Huduma Jumuishi za Uchukuzi, Ufadhili Endelevu na Uwajibikaji wa Sekta kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” unalenga kutathmini utekelezaji wa miradi na programu za sekta ya uchukuzi, kubaini mafanikio na changamoto pamoja na kuweka mikakati ya kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma.


EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"