WAFANYABIASHARA WA COMORO WAVUTIWA NA UFANISI WA UHUDUMUAJI SHEHENA BANDARI MTWARA
Bandari ya Mtwara imeendelea kupokea wageni mbalimbali ambapo tarehe 30 Aprili, 2026 imepokea ugeni wa wafanyabiashara kutoka Visiwa vya Comoro. Ugeni huo uliongozwa na Balozi wa Comoro Nchini Tanzania Dkt. Ahamada El Badaoui Mohamed.
Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kuwatambulisha rasmi wafanyabiashara hao kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) pamoja na kuomba ushirikiano katika kuhudumia meli za saruji zitakapowasili katika Bandari ya Mtwara.
Kufuatia ziara hiyo, wafanyabiashara hao wamebainisha kuwa kwa sasa Serikali ya Comoro inaendelea na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa viwanja vya michezo na hospitali jambo linaloongeza mahitaji makubwa ya saruji Nchini Comoro. Aidha, walieleza kuwa kwa sasa wanatumia saruji kutoka Kiwanda cha Dangote ambapo saruji hiyo inasafirishwa kupitia Bandari ya Mtwara kwa zaidi ya tani 10,000 kwa mwezi.
Kutokana na mahitaji hayo, wameomba TPA kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu katika kuhakikisha meli zinazobeba saruji zinahudumiwa kwa ufanisi na kwa wakati.
Katika ziara hiyo, wageni hao walipata fursa ya kutembelea miundombinu ya Bandarini hususan katika eneo la gati jipya na la zamani pamoja na ghala linalotumika kuhifadhi saruji ambapo walishuhudia shughuli za upakiaji zikiendelea kutekelezwa.
Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara Bw. Mtunze M. Sudi alielezea kuwa, maboresho yaliyofanyika katika Bandari ya Mtwara ikiwemo miundombinu na ununuzi wa mitambo imeongeza ufanisi katika utoaji huduma pamoja na utayari wa Bandari kuhudumia mizigo ya aina mbalimbali kwa wakati wote.
Katika hitimisho la ziara hiyo, wageni hao walieleza kuridhishwa na uwezo wa Bandari ya Mtwara baada ya kupata maelezo ya kina na kujionea namna shughuli mbalimbali za bandari zinavyotekelezwa kwa ufanisi mkubwa.


EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"