Select your language

Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abed Gallus Abed kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw. Plasduce Mbossa, tarehe 26 Oktoba, 2026 amefanya ziara ya kuwatembelea na kuwazawadia tuzo na vyeti wadau wake ikiwa ni kutambua mchango wao katika ufanisi wa bandari na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bw. Gallus amesema, tuzo hizi ni kielelezo cha kutambua kwamba mafanikio ya Bandari ya Dar es Salaam yanatokana na juhudi za wadau mbalimbali na ushirikiano wanaoutoa kwa viongozi wa TPA ili kufikia malengo ya uhudumiaji shehena.

Akipokea tuzo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Bw. Mohamed M. Salum , Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TASAC CPA. Pascal Karomba, ameipongeza TPA kwa ufanisi mkubwa na kusema Taasisi yake imekuwa ikitoa miongozo ambayo TPA imefanyia kazi na kufikia mafanikio na ufanisi mkubwa.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA) Bw. Edward Urio amewashukuru viongozi wa TPA kwa kutoa ushirikiano mkubwa kwa TAFFA na kusema mara nyingi viongozi hao wamekuwa wabunifu na wanachukua hatua kwa haraka.