TPA YASHIRIKI MAONYESHO YA BIASHARA NA UWEKEZAJI NYANDA ZA JUU KUSINI (KUSINI TRADE FAIR 2026)
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kupitia Bandari za Mtwara na Kyela, inashiriki katika Maonyesho ya Biashara na Uwekezaji Nyanda za Juu Kusini (Kusini Trade Fair 2026), yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Gondwe, eneo la Uyole, jijini Mbeya, kuanzia tarehe 16 Oktoba hadi 25 Oktoba 2026.
Maonyesho hayo yalifunguliwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mh. Solomon Itunda, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, yakiwa na lengo la kukuza biashara, uwekezaji na kuhamasisha matumizi ya fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo nchini.
Katika kipindi cha maonyesho hayo, viongozi mbalimbali, akiwemo Mkuu wa Wilaya, pamoja na wadau wa biashara na uwekezaji, wametembelea banda la TPA na kupata fursa ya kujifunza kuhusu huduma zinazotolewa na Bandari za Tanzania, pamoja na fursa mbalimbali za kibiashara zinazopatikana kupitia sekta ya bandari.
Wadau waliotembelea banda hilo wameonesha kufurahishwa na huduma, maelezo na elimu iliyotolewa na wataalamu wa TPA. Aidha, wameahidi kuwa mabalozi wazuri kwa kuwahamasisha wafanyabiashara na wadau wengine kutumia bandari zetu, huku wakitambua mchango wa sekta ya bandari katika kurahisisha biashara, kupunguza vikwazo vya usafirishaji na kukuza uchumi wa taifa.
Ushiriki wa TPA katika maonyesho haya ni sehemu ya juhudi za kuendelea kuutangaza mtandao wa Bandari za Tanzania, kuongeza uelewa wa umma kuhusu huduma za bandari na kuimarisha ushirikiano na wafanyabiashara, wawekezaji na wadau wa sekta ya usafirishaji. Kupitia huduma bora na miundombinu inayoendelea kuboreshwa, TPA inaendelea kujipambanua kama mdau muhimu katika kukuza biashara na kuunganisha Tanzania na masoko ya kikanda na kimataifa.
Maonyesho hayo yanatarajiwa kuhitimishwa rasmi Jumapili, tarehe 25 Oktoba 2026, na Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Mbunge wa Jimbo la Uyole na Rais wa Heshima wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).
Kaulimbiu ya maonyesho hayo ni: “Wekeza Kusini mwa Tanzania, Lango la Afrika Mashariki na SADC.”

EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"