TPA, DP WORLD NA TEAGT WAFUNGUA FURSA MPYA ZA BIASHARA ZAMBIA
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kwa kushirikiana na waendeshaji, kampuni za DP World na Tanzania East Africa Gateway Terminal (TEAGT) wameendelea kuimarisha uhusiano na jumuiya ya wafanyabiashara nchini Zambia kupitia jukwaa la kuwashirikisha wateja lililofanyika Septemba 22 na 23, 2026.
Jukwaa hilo lililenga kuimarisha mahusiano yaliyopo na jumuiya ya wafanyabiashara wa Zambia, kuwasilisha mafanikio yaliyopatikana katika kuboresha huduma za bandari na kutafuta fursa mpya za biashara.
Shughuli hizo, zilizoandaliwa kwa pamoja na TPA, TEAGTL) na DP World, zilihusisha ziara za kimkakati kwa wateja, mikutano na wadau pamoja na majadiliano ya kibiashara kati ya wafanyabiashara na watoa huduma (Business-to-Business).
Ziara za kimkakati kwa wateja zilifanyika Septemba 22, 2026, ambapo ujumbe wa Tanzania ulikutana na wafanyabiashara na wadau mbalimbali nchini Zambia kujadili mahitaji yao, changamoto wanazokutana nazo na namna ya kuimarisha matumizi ya Bandari za Tanzania.
Siku iliyofuata, Septemba 23, 2026, mkutano wa wadau ulifanyika katika Hoteli ya Protea, Ndola, Zambia, ukiwakutanisha wawakilishi wa Serikali, taasisi za umma, waendeshaji wa vituo vya mizigo, kampuni za usafirishaji na jumuiya ya wafanyabiashara pamoja na vyama vya wafanyabiashara nchini Zambia
Ujumbe wa Tanzania ulihusisha TPA, waendeshaji wa vituo vya mizigo pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya usafirishaji na biashara, wakiwemo Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu (TASAC), Central Corridor, Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PBPA), Mamlaka ya Udhibiti wa Kemikali na Gesi (GCLA), Tanzania Shippers’ Association (TASAA), Tanzania Freight Forwarders Association (TAFFA), Tanzania Association of Clearing and Forwarding Agents (TACAS), Sinotaship na Tanzania Association of Transporters and Operators (TATOA).
Katika mkutano huo, ujumbe wa Tanzania uliwasilisha hatua mbalimbali zilizochukuliwa kuboresha ufanisi wa huduma za bandari, ikiwemo huduma kwa wateja na mifumo ya usafirishaji wa mizigo. Wadau wa Zambia walipata pia fursa ya kutoa maoni, kueleza mahitaji yao na kujadili maeneo ya ushirikiano wa kibiashara.
Majadiliano hayo yalilenga pia kutambua fursa mpya za biashara na kuimarisha ushirikiano kati ya wafanyabiashara wa Zambia na watoa huduma katika mnyororo wa usafirishaji kupitia Bandari za Tanzania.
Jukwaa hilo ni sehemu ya jitihada za TPA na wadau wake za kuongeza ushiriki wa Bandari za Tanzania katika soko la kikanda kwa kuimarisha uhusiano na nchi jirani, hususan Zambia, kupitia Ukanda wa Kati.
Kupitia ushirikiano huo, TPA na wadau wake wanalenga kuendelea kuboresha huduma, kukidhi mahitaji ya wateja na kuongeza matumizi ya Bandari za Tanzania kama lango la biashara kwa Zambia na nchi nyingine zinazotumia Ukanda wa Kati.


EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"