Select your language

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeipongeza Serikali kwa mabadiliko makubwa ya miundombinu yaliyofanyika katika Bandari ya Tanga na kuleta tija na ufanisi mkubwa katika kuhudumia Shehena.

 

Pongezi hizo zimetolewa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Prof. Joyce Ndalichako ( Mb) tarehe 13 Machi 2026, baada ya Kamati kutembelea na kukagua mradi wa maboresho wa Bandari ya Tanga.

 

“ Tunaipongeza sana Serikali kwa kazi kubwa na kiwango kikubwa cha mabadiliko kilichofanyika. Tumeona hakuna kuchelewa wala kukwama kwa huduma ya shehena, hakika mafanikio ni makubwa na mapato yameongezeka sana.” Amesema Mhe. Prof. Ndalichako.

 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile( Mb) ameishukuru Kamati kwa ziara yao iliyowawezesha kuona kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya sita katika maboresho makubwa ya miundombinu kwenye Bandari ya Tanga huku akiihakikishia kamati hiyo kuwa maoni, ushauri na maelekezo waliyoyatoa yatafanyiwa kazi.

 

Naye Mkurugenzi wa Mipango, ubora na vihatarishi Dkt. Boniphace Nobeji, akizungumza mbele ya Kamati hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA

 amesema, TPA inathamini ushirikiano inaoupata kutoka Serikalini unaopelekea kutekeleza mipango yake inayolenga kuboresha miundombinu na kuleta tija katika Bandari zote nchini.

 

Mapema akisoma taarifa ya maboresho ya Bandari ya Tanga kwa kamati, Meneja wa Bandari ya Tanga Bw. Salehe Mbega, amesema maboresho ya miundombinu yaliyofanyika katika Bandari ya Tanga yameleta tija na ufanisi mkubwa katika kuhudumia Shehena Bandarini hapo na hivyo kuchagiza ongezeko la makusanyo ya mapato ya Nchi.

 

Bw. Mbega ameieleza Kamati hiyo kuwa mipango iliyopo sasa ni kujenga gati mpya tatu za mita 900 , kwa kuanza na gati mpya moja ya mita 300 ili kuendelea kuongeza ufanisi wa utoaji huduma katika Bandari hiyo.