SERIKALI KUENDELEA KUWEKEZA KATIKA MIUNDOMBINU YA BANDARI NCHINI
Serikali imesema itaendelea kuwekeza katika bandari zake nchini kwa lengo la kupunguza gharama na muda wa usafirishaji, pamoja na kuimarisha usalama wa meli ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri wa majini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Mwakiposa Kihenzile (Mb.), wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Usafiri Majini Duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Kijiji cha 21, Mkoani Tanga.
Kihenzile alisema kuwa, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imeendelea kuwekeza na kuimarisha miundombinu ya bandari, huduma za mizigo na abiria, pamoja na usalama wa vyombo vya majini.
Aidha, Kihenzile alisema umuhimu wa sekta ya usafiri wa majini unaonekana pia katika mchango wake kwenye mapato ya Serikali, ambapo kuanzia mwaka wa fedha 2020/2021 hadi 2024/2025, kodi za forodha kutoka bandarini zilichangia wastani wa takribani asilimia 40 ya mapato yote ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Awali, akitoa maelezo mbele ya Mgeni Rasmi, Mwakilishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Meneja wa Bandari ya Tanga, Bw. Salehe Mbega Salehe, alisema kuwa ili bandari izidi kuongeza ufanisi, imechukua hatua za kuongeza wataalamu katika fani ya usafiri wa majini (Marine).
Alisema wafanyakazi 25 wamepelekwa nje ya nchi kwa ajili ya mafunzo katika fani mbalimbali zinazohusiana na sekta hiyo, ambapo wanatarajiwa kumaliza masomo yao mwaka 2027.
Kwa upande wa vifaa, Mbega alisema TPA imeongeza idadi ya vifaa na vyombo vya baharini, ikiwemo Tug Boat saba zenye teknolojia ya kisasa, pamoja na boti mbili kwa ajili ya kufanya doria katika ukanda wa Bahari ya Hindi na nyingine katika Ziwa Victoria.
Kwa upande wa shehena, Mbega alisema TPA imeongeza kiwango cha shehena iliyohudumiwa kutoka tani 32,753,618 katika mwaka wa fedha 2024/2025 hadi tani 39,898,913 mwaka 2025/2026, sawa na ongezeko la asilim ia 21.8.
Alisema kwa mwaka wa fedha 2026/2027, TPA inatarajia kuhudumia jumla ya tani 43,372,285 za shehena.


EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"