PR0F. MBARAWA ARIDHISHWA NA UBORA WA MRADI WA BANDARI YA MWANZA KASKAZINI
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mnyaa Mbarawa ( Mb), ameridhishwa na ubora wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi na uboreshaji wa Bandari ya Mwanza Kaskazini wenye thamani ya shilingi bilioni 18.6 huku akitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha kazi zilizobaki zinakamilika kwa wakati ili bandari hiyo ianze kutoa huduma zilizokusudiwa.
Prof. Mbarawa ameeleza kuridhishwa kwake na Mradi huo terehe 16 lNovemba, 2026, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo uliofikia asilimia 90 ya utekelezaji wake.
Ameipongeza TPA kwa usimamizi mzuri na ubora wa kazi zilizofanyika, akisisitiza kuwa hatua iliyofikiwa inapaswa kuendelezwa kwa kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kuanza kuwanufaisha wananchi.
Awali akitoa maelekezo ya mradi kwa Waziri Prof. Mbarawa kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Naibu Mkurugenzi Mkuu Mha. Dkt. Baraka Mdima amesema, Mamlaka inaendelea kusimamia utekelezaji wake ili kuhakikisha unakamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Amesema maboresho yanayofanyika katika bandari hiyo yameongeza kina cha maji kutoka mita tatu hadi tano, hatua itakayowezesha meli kubwa zaidi kutia nanga. Vilevile, urefu wa gati umeongezeka kutoka mita 350 hadi mita 700, jambo litakaloongeza uwezo wa bandari kuhudumia meli na kuboresha ufanisi wa huduma za usafirishaji katika Ziwa Victoria.
Mradi wa Bandari ya Mwanza Kaskazini ni sehemu ya uwekezaji wa Serikali katika kuboresha bandari za Ziwa Victoria, kuongeza uwezo wa kuhudumia mizigo na abiria pamoja na kuimarisha usafirishaji na biashara katika ukanda wa Ziwa Victoria.


EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"