Select your language

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeeleza dhamira yake ya kuunga mkono mipango ya kukuza uwekezaji, ubunifu, kubadilishana maarifa na kushirikiana na Wadau wa shughuli za kibandari katika ukanda wa Kusini na Mashariki mwa Afrika.

Kauli hiyo imetolewa tarehe 28 Oktoba,2026, na Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano Dkt.George Fasha kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, wakati akifungua Mkutano wa Uwekezaji na Maonesho yaliyoandaliwa na Chama cha Usimamizi wa Bandari ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika jijini Dar es Salaam.

Aidha Dkt. Fasha alisema PMAESA imebeba jukumu muhimu katika kuendeleza ushirikiano miongoni mwa bandari, korido za usafirishaji na wadau wa masuala ya bahari, na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika muunganisho wa kikanda, urahisishaji wa biashara na ukuaji wa uchumi.

Alisema kwa kupitia juhudi za pamoja, ufanisi wa shughuli za kibandari utaongezeka na kuimarisha uthabiti wa mifumo ya usafirishaji inayounga mkono agenda ya maendeleo ya Afrika.

Mkutano na Maonesho ya PMAESA unatarajiwa kuendelea mpaka Oktoba 30,2026 ambapo Wanachama kutoka nchi zaidi ya 10 wanashiriki katika majadiliano ya kuongeza uwekezaji katika shughuli za kibandari na usafirishaji fungamanishi.