Select your language

Meneja wa Bandari ya Mtwara, Bw. Ferdinand S. Nyathi, ameongoza kikao cha 40 cha Baraza la Wafanyakazi wa Bandari ya Mtwara kilichofanyika mjini Lindi.

Kikao hicho kililenga kujadili na kutathmini utekelezaji wa malengo ya Bandari ya Mtwara kwa kipindi cha nusu mwaka, kuanzia Januari hadi Juni 2026, pamoja na kujadili mipango na mikakati mipya ya Bandari ya Mtwara kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Katika kikao hicho, wajumbe walijadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya Bandari ya Mtwara, mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza na namna ya kuimarisha utendaji kazi ili kuongeza ufanisi na tija katika utoaji wa huduma za kibandari.

Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Nyathi aliwasisitiza wajumbe kuendelea kujipanga vizuri katika maeneo yao ya kazi, kuzingatia uwajibikaji na kuongeza ushirikiano ili kuhakikisha Bandari ya Mtwara inaendelea kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wateja na wadau wake. Alisisitiza umuhimu wa maandalizi madhubuti katika kipindi hiki cha msimu wa usafirishaji wa korosho, ili kuhakikisha shehena zinahudumiwa kwa ufanisi na shughuli za bandari zinaendelea kwa kasi inayotarajiwa.

Aidha, aliwapongeza wafanyakazi kwa juhudi, ushirikiano na ufanisi waliouonesha katika kutekeleza majukumu yao, akibainisha kuwa mchango wao ni muhimu katika kufanikisha malengo ya Bandari ya Mtwara na kuimarisha huduma kwa wateja na wadau. 

Kikao hicho ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano, uwajibikaji na mipango ya maendeleo ya Bandari ya Mtwara, huku kikilenga kuongeza tija, kuboresha huduma na kuhakikisha bandari inaendelea kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi katika ukanda wa Kusini.