KAMATI YA SIASA YA WILAYA YATEMBELEA BANDARI YA TANGA
Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Tanga ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Meja Mstaafu Hamisi Mkoba imefanya ziara katika Bandari ya Tanga kwa lengo la kukagua hali ya utendajikazi wa bandari hiyo.
Akiongea mara baada kujionea hali ya utendajikazi wa bandari hiyo, Meja Mkoba aliipongeza Menejimenti kwa usimamizi mzuri wa fedha za serikali zilizoletwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika bandari hiyo.
“Mojawapo ya kazi ya kamati hii ni kupitia na kukagua miradi yote ya maendeleo katika Mkoa wetu, hivyo tumeridhishwa na mradi wa maboresho uliofanyika katika bandari hii”. Aliongeza Meja Mstaafu Mkoba.
Awali akitoa taarifa ya mradi wa maboresho yaliyofanyika bandarini hapo,Meneja wa Bandari ya Tanga Bw.Salehe Mbega alisema kuwa, maboresho hayo yamesaidia kutoka kuhudumia meli 110 kwa mwaka hadi meli 450 kwa mwaka.
Kwa upande wa shehena Bw. Mbega alisema kuwa kabla ya maboresho, bandari hiyo ilikuwa inauwezo wa kuhudumia shehena tani 400,000 tu kwa mwaka lakini baada ya maboresho imeweza kuhudumia mpaka shehena tani 1,300,000 kwa mwaka 2024/2025.
Aidha maboresho hayo pia yameongeza fursa za ajira kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga ambapo kwa ajira za kudumu kutoka watumishi 200 mpaka kufikia 344, na kwa upande wa wafanyakazi wa kutwa kutoka 6,000 hadi kufikia 17,000 kwa mwezi.
Katika hatua nyingine Bw. Mbega aliiambia kamati hiyo kwamba, serikali inatarajia kufanya mradi mwingine wa kuongeza gati 3 zenye urefu wa mita 900 ambapo utekelezaji wa awali umeshaanza kufanyika.


EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"