Select your language

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imeahidi kuongeza shehena inayopitia Bandari ya Dar es Salaam kufikia asilimia 60 kutoka asilimia 50 ya sasa kufuatia uchimbaji wa madini katika migodi mipya.  Hayo yamesemwa na Waziri wa Biashara ya Kimataifa wa DRC, Mhe. Julien Paluku Kahongya, mapema tarehe 19 Septemba, 2026 alipotembelea TPA pamoja na ujumbe wake wa viongozi waandamizi wa Serikali ya Kongo.  
Amesema serikali yake imejipanga kutumia fursa ya usafirishaji wa shehena kupitia mpaka mmoja kufika Bandari ya Kigoma ambapo Serikali ya Tanzania tayari imezindua meli kwa ajili ya kusafirisha shehena ya DRC.  

Ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuipatia DRC ardhi kiasi cha hekta 60 katika Bandari Kavu ya Kwala kwa ajili ya kuhifadhi shehena ya DRC kabla ya kusafirishwa kwenda nchini mwake. Aidha, amebainisha kuwa Serikali yake pia imetenga ardhi kiasi cha hekta 60 kwa ajili ya Serikali ya Tanzania ili kuwezesha shughuli za kiusafirishaji  huko DRC.  Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu TPA Bw. Plasduce M. Mbossa , Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abed G. Abed amemweleza Waziri huyo kwamba Serikali ya Tanzania inaboresha Bandari ya Kigoma kupitia Mwekezaji binafsi na kujenga reli ya SGR ili shehena kutoka DRC iweze kusafirishwa moja kwa moja kupitia mindombinu hiyo.