Select your language

Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Fatma Almas Nyangasa pamoja na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, tarehe 30 Septemba, 2026 wamefanya ziara katika Bandari ya Tanga kwa lengo la kujifunza na kuangalia fursa zinazopatikana katika Mkoa wa Tanga.

Akiongea na Menejimenti pamoja na Madiwani alioambatana nao, Mhe. Nyangasa, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa dhamira ya kuwekeza katika bandari nchini, akisema uwekezaji huo unaongeza tija na kuchangia maendeleo ya taifa.

“Tunampongeza Rais wetu kwa dhamira yake ya dhati ya kuwekeza katika Bandari ya Tanga na kuifanya bandari hiyo kufanya mambo makubwa yenye manufaa kwa taifa,” alisema Mhe. Nyangasa.

Katika ziara hiyo, Mhe. Nyangasa aliipongeza Menejimenti ya Bandari ya Tanga kwa usimamizi mzuri wa shughuli za bandari, akisema hali hiyo imechangia kuongezeka kwa shehena na mapato.

Awali, akitoa maelezo kuhusu maendeleo ya Bandari ya Tanga, Meneja wa Bandari hiyo, Bw. Salehe Mbega Salehe, alisema uwekezaji uliofanyika wenye thamani ya shilingi bilioni 429.1 umewezesha kuongeza idadi ya meli zinazohudumiwa kutoka meli 100 hadi 616 kwa mwaka.

Kwa mujibu wa Bw. Salehe, uwekezaji huo pia umewezesha Bandari ya Tanga  kutoka kuhudumia tani 400,000 hadi kufika tani 2,170,000 kwa mwaka.

Ongezeko hilo limeongeza shughuli za bandari na fursa mbalimbali za kiuchumi, hatua inayochangia kuimarisha mchango wa Bandari ya Tanga katika  kukuza biashara katika Mkoa wa Tanga na maendeleo ya taifa.