Select your language

Bandari ya Tanga inalenga kuongeza idadi ya meli, shehena na abiria pamoja na mapato katika mwaka wa fedha 2026/2027, sambamba na ununuzi wa mitambo na mafunzo kwa wafanyakazi kwa lengo la kuongeza ufanisi wa huduma.

Hayo yamebainishwa katika Kikao cha 40 cha Baraza la Wafanyakazi Bandari ya Tanga (Muster Workers Council ) kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani.

Kikao hicho kiliazimia kusimamia uboreshaji wa miundombinu ya Bandari ya Tanga ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa na Serikali yanafikiwa.

Akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho, Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Meneja wa Bandari ya Tanga, Bw. Salehe Mbega, aliwataka wafanyakazi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi, pamoja na kusimamia na kutunza ipasavyo vitendea kazi ili kufanikisha malengo yaliyowekwa na bandari.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Shughuli za Meli na Bandari  kituo cha Tanga (DOWUTA), Bw. Aliko Mwakipagala, aliwapongeza wajumbe wa Baraza hilo kwa kuungana pamoja na kupokea maazimio ya kikao, akisisitiza umuhimu wa kuyatekeleza ili kufikia malengo ya kituo.

Aidha, aliwahakikishia wafanyakazi kuwa chama kitaendelea kushirikiana nao katika kuhakikisha shughuli za bandari zinaendelea kutekelezwa kwa ufanisi.